Wanahabari Mkoa wa Morogoro waomba kujengewa uwezo zaidi, kwenye uandishi wa habari za lishe

News Image

Imewekwa: 3rd Aug, 2020

Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Morogoro (MOROPC) kimeiomba Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kuendelea kutoa mafunzo kwa waaandishi wa habari mkoani humo, ili kuzidi kuwajengea uwezo wa kuripoti habari mbalimbali zinazohusu masuala ya chakula na lishe.

Akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo wahariri na wanahabari wa mkoa wa Morogoro, namna ya kuhariri na kuandika habari zinazohusiana na Chakula na Lishe Mwenyekiti wa MOROPC, Nikson Mkilanya, amesema mkoa huo una zaidi ya waandishi wa habari 100, na 40 pekee ndio waliopatiwa mafunzo hayo, hivyo ameiomba Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kuendelea kutoa mafunzo hayo na kwa waandishi wengine mkoani humo.

Mkilanya amesema kwa muda mrefu waandishi wa habari mkoa wa Morogoro walikuwa na kiu ya kupata elimu kuhusu masuala ya Chakula na Lishe, hivyo ameishukuruTaasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kuwapatia mafunzo hayo.

“Tunaishukuru sana TFNC kwa kutupatia mafunzo haya wahariri na wanahabari wa Morogoro, kwani tunaamini mlikuwa na uwezo wa kuyapelekea mafunzo haya mkoa wowote, lakini mkaamua mje kwetu, hata hivyo tunaomba sana muendelee kutunoa, hususani katika lishe, kwani waandishi wengi mkoani hapa walikosa kabisa fursa ya kujengewa uwezo kwenye kada hiyo, ili kuwawezesha kuwa wabobezi” Alisema Mkilanya.

Mwenyekiti huyo pia ameiomba Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na Baraza la Habari Nchini, na kuingiza Kipengele cha Tuzo za Uandishi wa Habari za Lishe, kwani kufanya hivyo kutaongeza chachu kwa wanahabari kuandika zaidi habari zinazohusu masuala ya Chakula na Lishe, ambayo yatasaidia kutoa elimu kwa Jamii.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro Ester Kawishe ambaye alikuwa mwezeshaji akishirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, aliwaomba waandishi wa Habari kushirikiana na maafisa lishe waliopo katika Halmashauri zote za Morogoro, ili kufanikisha kutoa elimu sahihi ya lishe kwa wajamii nzima.

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imetoa mafunzo ya siku mbili kwa wahariri na waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro, ambayo yamelenga kuwajengea uwezo namna ya kuandika habari, makala na kuandaa vipindi, pamoja na kuelezwa wajibu wa wanahabari katika kushiriki kwenye kutoa elimu ya lishe.