Historia ya Taasisi
Nchini Tanzania shughuli za lishe zilianzishwa na Wizara ya Afya mnamo miaka ya 1950 kutokana na ripoti zilizoonyesha ongezeko la ukubwa wa vifo, ongezeko la magonjwa mbalimbali, tukio la njaa na uwepo wa vichocheo vingine ambavyo vilichangia ukuaji wa udumavu. Jitihada kubwa zilichukuliwa katika kupambana na kila hali kama vile kuzorota kwa hali kubwa ya afya katika idadi ya kundi la aina fulani la watu. Zaidi ya hayo mfumo wa ushirikiano wa sekta-mtambuka ilitumika na kupelekea maendeleo ya kuundwa kwa Kamati ya Ushauri ya Sekta-Mtambuka lengo lake kuu lilikuwa ni kutoa ushauri katika masuala mbalimbali ya lishe.
Baada ya uhuru, mchango mkubwa wa kisiasa katika masuala ya lishe, ulikuwa muhimu katika kuendeleza shughuli za lishe nchini. Mwaka 1963, Mhe. Rais Julius K. Nyerere alitangaza dhima ya Serikali katika kupambana na utapiamlo. Hii ilipelekea mwaka 1966, kuanzishwa kwa shule ya kwanza inayofundisha masuala ya lishe, shule hii ililenga kuwajengea uwezo wauguzi, maafisa ustawi wa kilimo, maafisa ustawi wa jamii na walimu. Azimio la Arusha lililopitishwa mwaka 1967 likaja kusisitiza mapambano dhidi ya udumavu kwa makundi maalumu katika ngazi zote. Hivyo Jitihada hizi zikapelekea idara mbalimbali kufanya shughuli za lishe, na ishara ya muingiliano wa kimajukumu ikaanza kuonekana.
Kwa mantiki hiyo, kazi nyingi za lishe zilikuwa zinafanyika bila ya kuwa na taasisi yenye mamlaka kisheria ya kuongoza na kusimamia masuala ya lishe. Hali hii ikapelekea kuibuliwa kwa wazo la kuanzisha Taasisi inayojitegemea ya Chakula na Lishe kwa ajili ya kuratibu shughuli zote za chakula na lishe, wazo ambalo liliungwa mkono na watu wengi nchini waliokuwa wanafanya shughuli za lishe. Hivyo ikaundwa timu chini ya usimamizi wa SIDA iliyopewa jukumu la kuunda muundo wa taasisi hiyo, timu hiyo ilimaliza kazi yake mwaka 1972 ambapo ilipendekeza sekta zaidi zihusishwe. Muundo huo ulipitishwa na kufanikisha kuunda Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania(TCLT) chini ya Sheria ya bunge Na. 24 ya mwaka 1973. Mwaka 1974 Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania ilizinduliwa rasmi chini ya Wizara ya Kilimo, baadae ikahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kisha Wizara ya Afya.