Mpango wa Pili Jumuishi wa Taifa wa masuala ya Lishe

Bonyeza hapa kupakua Mpango wa pili Jumuishi wa Taifa wa masuala ya Lishe (NMNAP II)_Swahili

Mpango wa pili Jumuishi wa Taifa wa masuala ya Lishe (NMNAP II) umeandaliwa ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa afua za lishe nchini kwa kipindi cha miaka mitano yaani 2021/22 – 2025/26. Mpango huu wa miaka mitano unazingatia ushahidi wa kitaalam unaolenga kuimarisha mikakati ya kukabiliana na aina zote za utapiamlo kwa watu wa rika mbalimbali na kujumuisha pia watu wenye mahitaji maalum hapa Tanzania Bara. Mpango huu unafuatia mpango wa awali uliokuwa ukitekelezwa kwa kipindi cha 2016/17 – 2020/21, na umebuniwa kwa kuzingatia pia mafanikio, mapungufu na fursa zilizobainishwa kwa miaka mitano iliyopita ya utekelezaji. Mpango huu wa pili unalenga afua za lishe zinazohusu hatua zote za makuzi ya binadamu tungu mimba kutungwa na utekelezaji utafanyika kupitia mifumo ya kisekta, kuendeleze ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau wote muhimu na kuhamasisha ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi katika kukabiliana na visababishi vya utapiamlo katika jamii. Matokeo ya jumla yanayotarajiwa (Nadharia ya Mabadiliko) katika mpango huu ni Wanawake, Wanaume, Watoto na Vijana Balehe nchini Tanzania wanakuwa na hali bora ya lishe na wanaishi wakiwa na afya njema na hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa tija zaidi”.

Mpango huu wa pili (kwa upande mmoja) unawalenga watunga sera na watoa maamuzi katika ngazi zote – Taifa, Mkoa hadi ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika ngazi ya utekelezaji, mpango unawalenga wale wanaohusika na utekelezaji wa afua za lishe, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), Washirika wa Maendeleo (DPs), Asasi za Kiraia (CSOs), na sekta binafsi. Mpango huu pia utasaidia umma kwa ujumla kuelewa msimamo wa Serikali na hivyo kujua mwelekeo wake katika kuhakikisha lishe bora kwa Watanzania wote. Zaidi ya hayo, mpango huu una maeneo manne makuu ya ya matokeo tarajiwa, ambapo matatu ya kwanza ni yale yanayolenga moja kwa moja kushughulikia aina kuu tatu za matatizo ya utapiamlo, huku eneo la mwisho linalenga kuweka mazingira wezeshi kuwezesha utekelezaji madhubuti wa afua za lishe zilizopangwa (kwa kuzingati aina kuu tatu za matatizo ya utapiamlo). Kwa hivyo, maeneo makuu ya matokeo tarajiwa ni kama ifuatavyo:

Eneo 1: Kupungua kwa Utapiamlo

Eneo 2: Kupungua kwa tatizo la Upungufu wa Vitamini na Madini

Eneo 3: Kupungua kwa tatizo la Uzito Uliozidi na Kiribatumbo

Eneo 4: Kuimarika kwa Mazingira Wezeshi kusaidia utekelezaji wa afua za lishe

Kwa lengo la kufikia malengo na matokeo tarajiwa, mpango utajikita katika kufikiwa kwa matokeo matano (5) ya kimkakati ambayo yalitokana na “Nadharia ya Mabadiliko” ya mpango. Matokeo haya ni:

1.Kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa huduma za kutosha za lishe; zenye ubora na kwa uwiano sawa kwa watu wote katika ngazi ya jamii na vituo vya kutolea huduma.

2.Uwepo wa mabadiliko ya tabia ambao unasaidia katika kuimarisha hali za lishe za wahusika miongoni mwa Wanawake, Wanaume, Watoto na Vijana balehe.

3.Uwepo wa Mifumo endelevu ya chakula ambayo inayokidhi mahitaji ya mlaji kilishe.

4.Kuimarika zaidi kwa ushiriki na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali na sekta binafsi katika masuala ya lishe.

5.Mazingira wezeshi (sera, sheria na mifumo ya kutosha) ambayo yanasaidia upatikanaji na matumizi ya rasilimali watu na fedha zinazohitajika kwa ajili ya masuala ya lishe.

Ufuatiliaji na tathmini (M&E) katika utekelezaji wa mpango huu na utoaji wa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya utekelezaji itakuwa ni mchakato endelevu katika kipindi chote cha miaka mitano.Aidha, Mapitio ya Muda wa Kati (Mid Term Review) yatafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024, ili kujua hatua iliyofikiwa katika miaka miwili ya utekelezaji, na kupendekeza marekebisho (ikibidi) katika mikakati, afua, kazi au malengo yanayotarajiwa. Mapitio ya muda wa mwisho (End Time Review) yatafanyika mwaka wa 2026 kutathmini hali ya utekelezaji wa jumla wa mpango na kutumia mambo ambayo tutajifunza kutokana na utekelezaji ili kusaidia katika maandalizi ya mpango wa kitaifa unaofuata.


Mpango wa Kwanza Jumuishi wa Taifa wa masuala ya Lishe (NMNAP I)

Bonyenza hapa kupakua Mpango wa Kwanza Jumuishi wa Taifa wa masuala ya Lishe (NMNAP I)