Wapeni watoto wenu mlo wa asubuhi kabla ya kwenda shule

News Image

Imewekwa: 19th Nov, 2025

Wazazi na walezi wameaswa kuhakikisha wanawapatia watoto wenye umri wa kwenda shule mlo wa asubuhi kabla hawajaenda shule. Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Eshter Nkuba wakati akizungumza na wazazi na walezi wa shule ya msingi Unubini iliyopo manispaa ya Temeke.

Dkt. Nkuba amesema ni muhimu watoto kupewa mlo wa asubuhi nyumbani ili kumuwezesha asikae na njaa muda mrefu, kwani njaa humpunguzia mtoto umakini wa kusikiliza darasani na hivyo kushidwa kuelewa na kupokea maelekezo atakayopewa na walimu wake.

“Muda wa asubuhi akili ya binadamu hufanya kazi kwa umakini zaidi, ndio maana vipindi vingi vya hesabu shuleni hupangwa muda huo ili kumuwezesha mtoto kupokea na kuelewa kwa urahisi. Lakini mtoto huyo kama atatoka nyumbani asubihi bila ya kula chochote basi atasikia njaa na hivyo ubongo wake kutofanya kazi kwa ufanisi, na matokeo yake mtoto atasinzia darasani ama kukosa umakini wa kumsikiliza mwalimu”

Aidha Dkt. Nkuba amewaomba wazazi pia kuendelea kushirikiana na shule katika kuhakikisha watoto wao wanapata chakula cha mchana shuleni kwani njaa si rafiki wa masomo shuleni.

Kwa Upande wake Afisa Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi Manispaa ya Temeke, Mwalimu Donasiana Njuu akimwakilisha Afisa Elimu Manispaa ya Temeke amesema kuwa mpango wa kuwapa watoto chakula cha mchana ni mpango wa kitaifa uliowekwa na Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora katika mazingira mazuri bila ya kuwepo kwa kizuizi chochote.

“Mpango wa kuwapa watoto chakula cha mchana shuleni si mpango wa Unibini pekee, bali ni mpango wa kitaifa unatekelezwa nchi nzima kupitia waraka wa elimu bure wa mwaka 2016 unaoelezea majukumu ya mzazi ikiwemo kuwanunulia vifaa vya shule kama vile sare za shule na madaftari, lakini pamoja na kuwapatia chakula cha shule”. Amesema Mwalimu Njuu.

Awali wakati akielezea umuhimu wa kuwapa chakula wanafunzi shuleni, Afisa Lishe Mtafiti kutoka TFNC, Eliasaph Mwana amesema kuwa bado kumekuwa na mwitikio mdogo miongoni mwa wazazi katika kuchangia chakula shuleni jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa chakula. Mwana amesema takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 100 ni wanafunzi 56 tu ndio wanaopata chakula shuleni.

Mwana amesema kutoka na changamoto hiyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), pamoja na TFNC wameanzisha mradi wa Afya na Lishe Mashuleni ili kuhakikisha kila mwanafunzo anapata chakula shuleni. Mradi huu unatekelezwa katika shule 15 za msingi katika manispoaa ya Temeke ambazo ni; Lioness Miburani, Unubini, Likwati, Madenge, Charambe, Chemchem, Nzasa, Kilamba, Marten Lumbanga, Amani, Bokorani, Ali Hassan Mwinyi, Mabatini, Umoja na Kibasila