Umuhimu wa kunyonyesha mara baada ya kujifungua

Watoto wachanga wanapaswa kuanza kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa ili maziwa yaanze kutoka mapema. Inashauriwa mara baada ya kujifungua mama na mtoto wagusane ngozi kwa ngozi ili kusaidia maziwa kutoka na kuongeza uhusiano kati ya mama na mtoto. Ni muhimu kwa mtoto kuwekwa kwenye titi ili aanze kunyonya maziwa ya mama.

Mama na mtoto wasitenganishwe, wawe pamoja muda wote, ila wanaweza kuteganishwa kwa ushauri wa dakatari ikiwa kuna tatizo litakalomuathiri mtoto akiwa na mama yake mfano ugonjwa wa mtoto au mama.

Kumnyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa kuna faida nyingi ikiwemo:

  • Kusaidia maziwa ya mama kuanza kutoka mapema na mtoto kupata maziwa ya mwanzo ya njano.
  • Kusaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali yake ya awali na kupunguza kutoka damu nyingi baada ya kujifungua.
  • Kusaidia kumpa mtoto joto
  • Kujenga uhusiano wa kihisia na upendo kati ya mama na mtoto
  • Kusaidia kuchochea maziwa kutoka kwa wingi

Umuhimu wa maziwa ya njano kwa mtoto

Maziwa ya njano ni maziwa ya mwanzo, mazito yenye rangi ya njano ambayo hutoka siku chache za mwanzo baada ya kujifungua. Maziwa haya ni chakula kamili chenye virutubishi vingi, na pia yanatoa kinga maalum dhidi ya maradhi.

Aidha maziwa ya njano humsaidia mtoto kutoa kinyesi cha mwanzo chenye rangi ya kijani au nyeusi ambacho humfanya mtoto aumwe tumbo siku za mwanzo kama hatanyonya