Ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha dhidi ya magojwa sugu ya figo

Kila alhamisi ya wiki ya pili ya mwezi Machi dunia huadhimisha siku ya figo duniani. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2006 katika nchi 66 na baadae kuenea katika nchi zote duniani. Nchini Tanzania siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 2011.

Lengo la kuadhimisha siku hii ni kufanya kampeni ya kidunia inayolenga kuongeza ufahamu kwa watu juu ya umuhimu wa figo na kuwahamasisha kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya maradhi ya figo (magonjwa sugu ya figo) na matatizo mengine ya kiafya yanayohusiana na figo.

Siku ya figo duniani tangu kuanza kwake hadi leo hii imekuwa ikiadhimishwa kwa kauli mbiu mbalimbali ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema:

Afya ya figo kwa kila mmoja kila mahali”

Magonjwa sugu ya figo ni moja wapo ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo pamoja na sababu nyingine yanayohusiana pia na ulaji usiofaa na mitindo ya maisha isiyosahii. Magonjwa haya huingia katika mwili wa binadamu kimya kimya bila ya kuonesha dalili za awali, dalili hujitokeza ugonjwa ukishakomaa aidha katika hatua ya kwanza na kuendelea. Hivyo ni vyema kila mmoja akajenga tabia ya kufanya uchunguzi wa figo mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu.

Ili kujikinga na kuzuia madhara yatokanayo na figo ni vema jamii ikachukua tahadhari kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  • Fanya mazoezi mara kwa mara angalau kwa muda wa dakika 30 kila siku
  • Zingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko kwa kiasi kulingana na mahitaji ya mwili wako na kazi unazozifanya
  • Dhibiti uzito wa mwili kwa kufanya mazoezi na kuepuka vyakula vilivyopikwa kwenye mafuta mengi na vinywaji vilivyoongezwa sukari (soda aina zote, juice za makopo)
  • Epuka uvutaji wa sigara na mazao yote ya tumbaku kwani husababisha mishipa kusinyaa
  • Epuka matumizi ya dawa za maumivu (brufen, diclopar, diclofenac ) pasipokuwa maelezo ya daktari
  • Kunywa maji mengi na ya kutosha angalau lita moja na nusu kwa siku
  • Fanya uchunguzi wa figo angalau mara moja kwa mwaka

Aidha kwa watu wenye ugonjwa wa figo wanashauriwa kuzingatia mambo yafuatayo

  • Dhibiti magojnjwa ya kisukari kwa kufuata ushauri na matumizi ya dawa kama alivyokuelekeza mtaalam wa afya
  • Zingatia ulaji unaofaa, na epuka kukaa na njaa
  • Dhibiti shinikizo la damu kwa kufuata ushauri na dawa kama alivyoelekeza daktari
  • Pata matibabu sahihi ya ugonjwa wa mawe kwenye figo na kuvimba tezi dume
  • Dhibiti kiwango cha maji na vimiminika vingine kama ilivyoshauriwa na daktari
  • Epuka matumizi ya chumvi