Umuhimu wa maji mwilini

Maji si sehemu ya kundi la chakula lakini maji yana umuhimu kubwa sana kiafya katika kufanikisha kazi mbalimbali mwilini. Pia viungo vingi vya mwili ili iweze kufanya kazi vizuri vinahitaji maji na zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwili wa binadamu ni maji. Hivyo maji husaidia mwili kufanya kazi mbalimbali na hii ni pamoja na;

  • Maji husaidia katika uyeyushwaji wa chakula, usafirishaji wa virutubishi na ufyonzwaji wa virutubishi mwilini.
  • Maji husaidia katika kutengeneza maji maji yanayopatikana katika viungo vya mwili kama vile viwiko na magoti, hivyo kusaidia viungo hivyo viweze kufanya kazi vizuri.
  • Maji hurekebisha joto la mwili.
  • Maji husaidia kuzuia kuondoa uchafu na mabaki ya uchafu mwilini kwa njia ya jasho na mkojo
  • Maji husaidia kupunguza uchovu wa mwili
  • Maji husaidia kuzuia uwezekano wa kupata baadhi ya magonjwa kama vile saratani ya tumbo na kibofu cha mkojo, na mawe kwenye figo hasa yanaponywewa kwa kiasi kinachotakiwa.

Kwa mtu mzima anashauriwa kunywa maji safi na salama kiasi cha lita moja na nusu kwa siku au glasi nane kwa siku. Pia mtu mzima anaweza kuongeza kiasi cha maji kwa kunywa kwa kutumia vitu vya majimaji kama vile supu juisi ya matunda halisi na madafu.

Watoto walioanza kupewa chakula wenye umri kuanzia miezi 6 na kuendelea wapewe maji kulingana na uhitaji wao na ni vyema wapewe maji baada ya kula na siyo kabla ya kula. Lakini kwa watoto wachanga wenye umri chini ya miezi 6 hairuhusiwi kiafya kupewa chakula na kinywaji chochote zaidi ya maziwa ya mama kwani maziwa ya mama yanavirutubishi na maji ya kutosha kulingana na mahitaji ya mtoto.

Namna mwili unavyopoteza maji mwilini

  • Joto kali: wakati wa joto kali mtu anakuwa kwenye hatari ya kupoteza maji kwa wingi mwilini kama hatokunywa maji ya kutosha kwa sababu wakati wa joto kali mtu hutokwa na jasho jingi hali ambayo huchangia maji kupungua.
  • Kuhara na kutapika: mtu anapokuwa katika hali hii maji mengi hipotea mwilini hivyo inashauriwa kunywa maji mara kwa mara ili kuzuia upungufu wa maji mwilini. Suala la kutumia maji yaliyoongezwa chumvi chumvi na sukari ni muhimu pia wakati mtu anapokuwa anaharisha, kutapika au anahalisha na kutapika kwa wakati mmoja.
  • Unywaji wa pombe kupita kiasi: kwa sababu pombe inasababisha mtu kwenda haja ndogo mara kwa mara na hivyo kupoteza maji kwa wingi.

Zingatia:

kunywa maji safi na salama ili kulinda afya yako. Takasa maji ya kunywa kwa kuyachemsha au kwa kuweka dawa ya waterguard kwani unywaji wa maji yasiyosafi na salama huweza kusababisha mtu kupata magonjwa ya kuharisha kama vile typhoid na kipindupindu.