LISHE SI SUALA LA KIAFYA PEKEE, BALI NI NGUZO YA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU, UCHUMI NA JAMII- MAJALIWA

News Image

Imewekwa: 30th Sep, 2025

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora”

Amesema hayo leo Jumanne (Septemba 30, 2025) wakati alipofunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC uliopo Bunju Jijini Dar es salaam.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara wa mapambano dhidi ya utapiamlo kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele kwa kuimarisha bajeti, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na uhamasishaji wa afua za lishe kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.

“Jitihada hizi zilimuwezesha kupata tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates Foundation, kutokana na mchango wake mkubwa katika kusukuma mbele Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan kwenye afya ya mama, mtoto na lishe”.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zote za umma na binafsi kutenge rasilimali za kutosha kwa ajili ya afua za lishe na kuziweka katika mipango yao ya kila mwaka ili kuongeza uwajibikaji na uendelevu katika kutekeleza mipango iliyopangwa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu)Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa wadau wote walioanishwa katika Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe wanaendela kutekeleza majukumu yao. "Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa Wizara zote zinaingiza masuala ya lishe katika mipango ya kibajeti kila mwaka.