Jitihada za pamoja zinahitajika kupambana na Udumavu – Dkt. Yonazi

News Image

Imewekwa: 2nd Aug, 2025

Dar es Salaam, Julai 28, 2025

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, ametoa wito kwa Serikali na wadau kushirikiana kwa karibu katika mapambano dhidi ya utapiamlo nchini.

Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe nchini, unaotarajiwa kufanyika Septemba 4–5, 2025 jijini Dar es Salaam, Dkt. Yonazi amesema juhudi za pamoja, tafiti, elimu na majukwaa ya kitaifa ni muhimu katika kutokomeza utapiamlo.

“Tunahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wadau kuhakikisha tunapunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya udumavu kupitia sera, elimu na programu zenye tija,” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna, amesema mkutano wa mwaka huu utaambatana na Lishe Marathon, yenye lengo la kuhamasisha afya bora kwa jamii na kuongeza uelewa wa masuala ya lishe.

Mkutano huo wa kitaifa unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.