Wadau, serikali tushirikiane kuimarisha lishe nchini

News Image

Imewekwa: 25th Jul, 2025

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dkt. Ntuli Kapologwe, amewataka wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini. Dkt. Kapologwe ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubushi kwenye Vyakula Tanzania (TFFA) unaofanyika jijini Arusha.

Dkt. Kapologwe amesema kuwa ECSA-HC itaendelea kushirikiana na TFFA ikiwa ni kuunga mkono jitihada za jukwaa hilo pamoja na Serikali katika utekelezaji wa afua mbalimbali za kilishe hususani kwenye suala la uongezaji wa viritubishi kwenye vyakula. “ili kuipa lishe kipaumbele mnaweza kuona hata sisi katika mpango mkakati wetu wa miaka 10, lishe ni moja ya malengo tisa yaliyoingizwa katika mpango mkakati wetu, lengo likiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa afua za lishe nchini” Amesema Dkt. Kapologwe.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dkt. Otilia Gowele akiwasilisha salamu za Wizara ya Afya katika Mkutano wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini Tanzania (TFFA), unaofanyika kwa muda siku mbili jijini Arusha ukiwakutanisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya urutubishaji wa vyakula wakiwemo kutoka Wizarani, Taasisi za Serikali, Vyuo Vikuu, Mashirika ya Maendeleo pamoja na wadau wengine.

Dkt. Gowele amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau wengine katika eneo la urutubishaji wa vyakula kwani ni eneo ambalo likiwepewa kipaumbele litasaidia kutatua changamoto ya tatizo la upungufu wa Vitamini na madini ambalo bado linaendelea kusumbua katika baadhi ya maeneo

Mratibu wa programu ya kuzuia upungufu wa madini joto Bi Rose Msaki wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) akiwasilisha taarifa ya Utafiti unaolenga kuangalia mfumo wa Sekta ya Afya kupima kiwango cha madini joto katika chumvi na mkojo, wakati Mkutano wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini Tanzania (TFFA), unaofanyika Jijini Arusha.

Bi. Msaki amesema kukamilika kwa utafiti huu unaotekelezwa na TFNC kwa kushirikiana na Shirika la Iodine Global Network, kunatajwa utaiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza Afrika kupima hali ya viwango vya madini joto katika jamii kwa kwa wakati kwa kutumia mifumo endelevu badala ya kusubiri tafiti za kitaifa zinazofanyika kila baada ya miaka mitano.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa TFFA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la SANKU Bw. Gwao Omari Gwao, amesema Jukwaa hilo limekutana kwa mara ya 39 tangu kuanzishwa kwake, lengo kubwa likiwa kuwakutanisha wadau na kujadiliana changamoto mbalimbali katika eneo la urutubishaji.

“Jukwaa hili linatukutanisha wadau mbalimbali pamoja na Serikali, ambapo kupitia mkutano huu tutaweza kutengeneza mpango mkakati wa pamoja wa miezi sita, ambao utaeleza maeneo ya kimkakati tunayotarajia kuyatekeleza kwa pamoja” Amesema Gwao.

Mtaalamu wa lishe Bi Joyce, kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF)akiwasilisha salamu za wadau wa maendeleo, na kuelezea namna shirika hilo walivyo mstari wa mbele katika kufadhili na kuendeleza utekelezaji wa afua za uongezwaji wa virutubishi kwenye chakula. Bi. Ngegba ameeleza hayo wakati wa Mkutano wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini Tanzania (TFFA), unaofanyika Jijini Arusha.

Afisa Mwandamizi wa mradi wa Urutubishaji wa Vyakula (Food Fortification) kutoka Shirika la kimataifa la Nutrition International (NI), Bi. Mariam Nakuwa, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Shirika hilo katika eneo la urutubishaji wa vyakula hususani kwenye eneo la uongezaji wa madini joto kwenye Chumvi, wakati wa Mkutano wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini Tanzania (TFFA).

Shirika la kimataifa la NI limekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania pamoja na wadau wengine katika eneo la urutubishaji hususani eneo la Chumvi, kwa kuhakikisha Chumvi inayozalishwa nchini inaongezwa madini joto ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa madini joto kwa jamii ya Watanzania.

Mkutano huo wa 39 wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini Tanzania (TFFA) utafanyika kwa muda Siku mbili jijini Arusha na umewakutanisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya urutubishaji wa vyakula wakiwemo kutoka Wizarani, Taasisi za Serikali, Vyuo Vikuu, Mashirika ya Maendeleo na wadau wengine.