Mwenge wa uhuru kutumika kueneza elimu ya Lishe

News Image

Imewekwa: 4th Oct, 2019

“Lishe bora ni msingi wa maendeleo, bila ya kuwa na lishe bora, afya bora hatuwezi kufikia lengo letu la kufikia uchumi wa viwanda” kauli hii imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (mb) wakati akifungua mkutano wa sita wa wadau wa lishe nchini katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma Oktoba 3, 2019.

Mhe. Waziri Mkuu amesema licha ya umuhimu wa lishe katika jamii lakini bado kumekuwa na changamoto kwa watu wengi kutozingatia kanuni za ulaji unaofaa na hivyo kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama kuhakikisha ujumbe wa lishe unawekwa kwenye mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2020.

“Ujumbe wa mwenge unaweza usiwe mmoja tu, unaweza kukusanya vitu viwili mpaka vitatu vikabeba kauli mbiu ya nchi, kwa hiyo mwakani tutaweka pia ujumbe wa lishe ili kila unapopita mwenge uweze kuwamulika watu na kuwahamasisha juu ya kuzingatia suala la lishe. Ni matumaini yangu kuwa elimu itawafikia watu wengi na tutapiga hatua kubwa katika masuala ya lishe”

Mkutano wa wadau wa lishe wa mwaka 2019 ni mkutano wa sita tangu mikutano hiyo ianze kufanyika mwaka 2014. Mkutano wa mwaka huu umejikita katika kutathimini utekelezaji wa Mpango Shirikishi wa Taifa wa Masuala ya Lishe unaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2021. Jumla ya washiriki 300 wamehudhuria mkutano huo wenye kauli mbiu “Matumizi ya Taarifa na takwimu za Lishe Katika Kuchochea Sera na Programu Kwa Maendeleo Endelevu Nchini Tanzania”.