TFNC yapongezwa kwa maandalizi ya wiki ya unyonyeshaji duniani

Imewekwa: 4th Apr, 2019
Kamati ya kitaifa ya lishe ya wajawazito, watoto wachanga, watoto wadogo na vijana balehe imeipongeza Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kwa kuanza mapema maandalizi ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani kwa mwaka 2019.
Kamati imetoa pongezi hizo wakati wa kikao cha kupitia utekelezaji wa shughuli za lishe ya wajawazito, watoto wachanga, watoto wadogo na vijana balehe kwa kipindi cha mwezi Januari 2019 hadi Machi 2019 kilichofanyika tarehe 04 Aprili, 2019 katika ukumbi wa TFNC.
“Kwa niaba ya kamati niipongeze TFNC. Hakika mwaka huu tunaona maandalizi yameanza mapema tofauti na miaka ya nyuma ambapo maandalizi kama haya yalikuwa yanafanyika mwezi juni hadi julai. Natumani kwa maandalizi haya mambo yataenda kuwa mazuri zaidi, kwa sababu kila mdau atakuwa na muda wa kujianda na kushiriki ipasavyo” amesema Tuzie Edwin, Mwenyekiti mwenza kutoka UNICEF.
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 01 hadi tarehe 07 Agosti duniani kote. Lengo la maadhimisho hayo ni kuelimisha na kuhamasisha jamii, wadau na serikali kuchukua hatua katika kutetea, kulinda na kuendeleza unyonyeshaji wa watoto wachanga na wadogo, na hivyo kuboresha hali ya lishe ya watoto.