TFNC yapata Mkurugenzi Mtendaji mpya

News Image

Imewekwa: 15th Jul, 2019

Dkt. Germana Leyna ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) akichukua nafasi ya Dkt. Vincent Assey ambaye amestaafu. Akimtambulisha mbele ya wafanyakazi wa taasisi hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya) Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Dkt. Leyna ni mchapakazi ndio maana Serikali imemteua kuiongoza TFNC katika kukabiliana na matatizo ya utapiamlo nchini.

“Haiwezekani mpaka sasa Tanzania tukawa na tatizo la udumavu, najua jitihada zimefanyika na kwa kiasi kikubwa tatizo limepungua lakini nia ni kuona tatizo hili linamalizika kabisa. Kama nchi sasa tunajenga viwanda ili kufikia uchumi wa kati, viwanda hivyo vinategemea nguvu kazi imara ili viweze kuendelea, hatuwezi kupata nguvu kazi kama watoto wetu wamedumaa. Ni changamoto kwenu kuhakikisha tatizo linaisha” amesema Dkt. Chaula.

Akiongea mara baada kukabidhiwa vitendea kazi Dkt. Leyna ameshukuru na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu kwa kushirikiana na wafanyakazi katika kuwatumikia wananchi ili kuhakikisha lengo la kutokomeza matatizo ya lishe nchini linafikiwa.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Leyna alikuwa ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).