Wadau wa lishe wakutana siku mbili

News Image

Imewekwa: 17th May, 2019

Wadau wa lishe nchini Tanzania wamekutana katika kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika Mei 15 na Mei 16, 2019 katika ukumbi wa Protea jijini Dar es salaam na kujadili namna ya kufanya mapitio ya kati ya utekelezaji wa mpango jumuishi wa kitaifa wa lishe wa miaka mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2021.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Ndg. Joseph Kiraia ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu amesema kuwa kikao hicho kimewakutanisha wadau wa lishe kutoka Wizara na Taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo. Katika kikao hicho washiriki walipewa jukumu la kufanya tathimini ya utekelezaji wa mpango huo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu ya utekelezaji.

“Tumeweza kupeana majukumu katika makundi matatu ambayo ni; kundi la wadau watakaotathimini masuala ya kujenga mazingira wezeshi; kundi la wadau watakaotathimini masuala ya utekelezaji wa afua za kukabiliana na sababu za moja kwa moja za utapiamlo; kundi la wadau watakaotahimini masuala ya utekelezaji wa afua za kukabiliana na sababu zilizojificha za utapiamlo. Baada ya makundi hayo kukamilisha majukumu yao, kazi zao zitajumuishwa pamoja ili kupata taarifa moja ya tathimini mnamo mwezi Agosti 2019” amesema Kiraia.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Dkt. Vincent Assey amesema kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwake mwaka 2016 mpango huu umefanikiwa kuwaweka pamoja wadau muhimu katika kushughulikia masuala ya lishe.

“Kabla hatujakuwa na mpango huu, shughuli za lishe zilikuwa zinatelezwa na sekta ya afya pekee, lakini baada ya kufanyika tathimini ikabainikika kwamba sekta ya afya inachangia asilimia 20 tu katika kuondoa matatizo yatokanayo na lishe duni, huku sekta nyingine zikiwa zinachangia kwa asilimia 80” amesema Assey.