Jumuiya ya watu wasioona Tanzania yakabidhi heti kwa WFP.

News Image

Imewekwa: 15th May, 2024

Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imekabidhi cheti cha pongezi kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), ikiwa ni kuthamini mchango uliotolewa na Shirika hilo katika kufanikisha utengenezaji wa nyenzo rafiki kwa watu wasioona kupata elimu ya masuala ya chakula na lishe kama ilivyo kwa wengine.

Akikabidhi cheti hicho kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WFP, Mwenyekiti wa TAB Bwa. Omary Itambu, amesema wametoa cheti hicho ikiwa ishara ya kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Shirika hilo kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, kuhakikisha watu wasioona nao wanafikiwa na elimu ya lishe kwa kuwapatia vitabu vya maandishi ya nukta nundu na Redio zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa kundi hilo.

Bwa. Omary amesema awali watu wasioona nchini walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa na elimu sahihi ya masuala ya lishe kutokana na aina ya ulemavu walionao na kujiona kama kundi ambalo limetengwa, hata hivyo baada changamoto hiyo kuifikisha TFNC, waliweza kushirikiana na WFP na kuhakikisha kundi hilo linapatiwa nyezo muhimu zitakazowasaidia kupata elimu sahihi ya lishe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, ameishukuru WFP kwa ushirikiano inaoendelea kuutoa kwa Taasisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kilishe, na kuiomba kuendelea kushirikiana zaidi katika kuyafikia makundi mengine maalumu ambayo bado yanahitaji elimu ya lishe kama ilivyofanya kwa watu wasioona.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi. Sarah Gordon- Gibson, ameipongeza Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania pamoja na Jumuiya ya Watu wasioona nchini, kwa ubunifu ulioufanya kuhakikisha jamii ya wasioona nao wanafikiwa na elimu ya lishe, na amejivunia kuona wao kama WFP wamekuwa sehemu ya kufanikisha jambo hilo, ambalo halikuweza kufanyika mahala pengine.