Serikali Kutunga Sheria ya Kuwatengea Bajeti ya Lishe Watoto Chini ya Miaka 5

News Image

Imewekwa: 14th Sep, 2018

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kwamba Serikali ina mpango wa kutunga sheria itakazozitaka halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Septemba 11, 2018 wakati akihutubia kongamano la wadau wa lishe nchini lililofanyika kwenye ukumbi wa kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa kwa sasa halmashauri zimeelekezwa kutenga kiasi cha shilingi 1,000/- kwa kila mtoto kutoka katika mapato yake ya ndani, lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa mpango huo kwa sababu ya kukosekana kwa sheria, hivyo baadhi ya halmashauri kulichukulia kama jambo la hiari.

“Lengo letu sasa fedha hii, isiwe inatolewa kwa matakwa ya halmashauri, wasiwe wanatoa kwa kadri wanavyojisikia. Tunahitaji liwe ni hitajio la kisheria, Serikali inakusudia kuweka sheria na halmashauri ni lazima watoe kiwango kitakachotamkwa, kupendekezwa na kupitishwa na wabunge”

Awali akieleza utekelezaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee Jinsia na Watoto katika masuala ya lishe, Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kupunguza tatizo la lishe duni kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano toka asilimia 42 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 34 mwaka 2015.

Aidha, Mhe. Mwalimu amesema kwamba licha na mafanikio hayo lakini bado Tanzania inakabiliwa na ongezeko la tatizo la lishe iliyozidi na vilibatumbo toka asilimia 22 hadi asilimia 28. Amesema sababu kubwa inayochangia kuongezeka kwa tatizo hili ni ulaji mbaya wa chakula pamoja na mfumo mbaya wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi, huku akiwataja watu wanaoishi mijini kuongoza kupatwa na tatizo hilo.

Kongamano la wadau wa lishe nchini hufanyika kila mwaka, ambapo kongamano la mwaka huu ni kongamano la tano tangu kuanza kwa makongamano hayo mwaka 2014. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Kuendeleza uchumi wa viwanda, lishe bora ni msingi wa kuendeleza nguvu kazi yenye tija”