Waajiri wanaozuia likizo za uzazi waache mara moja- Ummy Mwalimu

News Image

Imewekwa: 2nd Aug, 2019

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mb) amewataka waajiri binafsi wanaozuia likizo ya uzazi kuacha mara moja. Mhe. Waziri ametoa rai hiyo wakati akiongea na waandishi wa habari katika ufunguzi wa Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani 2019 uliofanyika 1 Agosti 2019 jijini Dodoma.

Mhe. Ummy amesema kwamba Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2017 mwanamke aliyejifungua ana haki ya kupewa likizo ya uzazi yenye malipo ya siku 84 akijifungua mtoto mmoja, na siku 100 kama atajifungua watoto mapacha. Pia amesema akimaliza likizo hiyo na kurudi kazini kifungu cha 33(10) kinampa haki ya kupata ruhusa ya masaa mawili kwa siku kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto. Ruhusa hiyo ya masaa mawili atakubaliana na mwajiri muda unaomfaa. Sheria hii pia humpa baba likizo ya siku 5 ndani ya wiki moja aliyojifungua mwenza wake.

“Sheria hizi zinafanya kazi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira, na Watu wenye Ulemavu inayoongozwa na Mhe. Jenister J. Mhagama. Lakini kwa kuwa masuala ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama yapo chini ya Wizara ya Afya, ninafikiria sasa pale wizarani kuwe na dawati la kupokelea malalamiko ya wafanyakazi waliozuiliwa likizo zao za uzazi ili tuweze kuwasaidia kufanya ufuatiliaji kwa maafisa kazi,

Awali akitoa neno la ukaribisho Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna amesema kuwa “unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa kuzingatia kanuni zake ikiwemo kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee miezi sita ya mwanzo kunafaida kubwa kwa mtoto, mama mwenyewe, jamii na taifa kwa ujumla”.

“Madhara ya kutonyonyesha maziwa ya mama yanahusishwa kudumaza maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili, pamoja na hasara nyingine za kiuchumi ambazo zinaweza kufikia kiasi cha dola bilioni 301 kwa mwaka” amesema Dkt. Leyna.

Kwa upane wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania Bwana James Gitau amesema maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani ni muhimu sana katika kuihamasisha jamii kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji.

“Umoja wa Mataifa unaipongeza sana Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kufanikisha unyonyeshaji nchini. Kauli mbiu ya mwaka huu inatukumbusha juu ya umuhimu wa kuwawezesha wazazi, na kuzingatia usawa wa kijinsia katika malezi ya watoto. Kama mama atasaidiwa na mwenza wake, familia, mwajiri na jamii kwa ujumla itazidi kumpa moyo na hivyo kusaidia unyonyeshaji kufanikiwa” amesema Gitau.

Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani hufanyika ulimwenguni kote kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti, ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Innocent la mwaka 1991 linalohusu kuwawezesha wanawake wote kunyonyesha maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo baada ya kujifungua. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Wawezeshe Wazazi: Kufanikisha Unyonyeshaji”.