WAJA- Tutaboresha hali ya lishe Ukerewe

News Image

Imewekwa: 2nd Oct, 2018

Watoa huduma katika ngazi ya Jamii (WAJA) wilayani Ukerewe wameahidi kuboresha hali ya lishe kwa watoto wachanga, watoto wadogo, wajawazito, wanaonyonyesha na wasichana balehe.

WAJA wametoa ahadi hiyo baada ya kupatiwa mafunzo ya mkoba wa siku 1000 yaliyofanyika 24-28 Septemba, 2018 katika ukumbi wa Umoja wilayani Ukerewe.

Akiongea kwa niaba ya wenzake Kweba Innocent amesema kuwa mafunzo waliyopewa ni muhimu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Mafunzo haya yametuongezea mbinu katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku. Mkoba huu wa siku 1000 ni nyenzo muhimu katika kufikisha elimu ya lishe kwa jamii kupitia vikundi shirikishi. Niishukuru Serikali kwa kutuletea huu mkoba, hakika imefanya kazi yake na sisi tutafanya kazi yetu kuhakikisha watu wanaelewa vyema dhana ya siku 1000” Amesema Kweba.

Mkoba wa siku 1000 unaelezea umuhimu wa lishe bora kwa mtoto chini ya miaka miwili (kuanzia mimba inapotungwa hadi atapotimiza miaka miwili baada ya kuzaliwa). Katika kipindi hiki mtoto anahitaji virutubishi zaidi ili kuendana na kasi ya ukuaji wake kimwili na kiakili.

Tafiti zinathibitisha kwamba mtoto akipata utapiamlo katika kipindi hiki, athari zake hazirekebishiki na anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari, baadhi ya saratani, na matatizo ya moyo atakapokuwa mtu mzima.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe, Sikitu Kihinga kutoka katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania amesema kuwa, mafunzo ya mkoba wa siku 1000 yametolewa kwa WAJA 535 katika mikoa mitano ya Mwanza, Kagera, Kigoma, Geita na Mara kwa ufadhili wa mradi wa USAID Boresha Afya