Watu 227 wapimwa hali zao za lishe wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani

News Image

Imewekwa: 4th Dec, 2019

Wananchi 227 wamejìtokeza kupima hali zao za lishe wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza katika viwanja vya Rock City Mall kuanzia tarehe 25/11/2019 hadi tarehe_ 01/12/2019.

Margareth Rwenyagira Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) amesema kuwa watu wengi waliojitokeza kupima wamefurahi kujua hali zao za lishe kwa sababu pia wamepata elimu na ushauri juu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha.

"Watu wengi waliokuja kupima walikuwa wanadhani kwamba mtu kuwa mnene ndio kuwa na lishe nzuri, na walikuwa hawajui juu ya ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha unaozingatia ulaji wa chakula unaotokana na makundi matano pamoja na kufanya mazoezi. Makundi hayo ya chakula ni kama vile; kundi la matunda, mbogamboga, jamii ya mikunde na asili ya wanyama, kundi la nafaka, mizizi na ndizi mbichi pamoja na kundi la mafuta sukari na asali ambalo linasisitizwa kuliwa kwa kiasi kidogo sana kwani chakula kilichopikwa kwa mafuta mengi na sukari nyingi vinaongeza uzito kwa haraka ha hivyo kumuweka katika hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani"

Lakini pia walikuwa hawajui umuhimu wa kula matunda na mbogamboga kwa wingi, hivyo baada ya kuwapima na kuwapatia elimu wameonesha kuelewa na kufurahia juu ya njia nzuri za kupunguza uzito kwa kuzingatia kanuni za ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha" amesema Rwenyagira.

Joygrace Shoo ambaye ni mmoja wa wanachi waliojitokeza kupima hali zao za lishe amesema kuwa elimu ya lishe aliyoipata imemfundisha mambo mengi ikiwemo kujua umuhimu wa lishe katika kujenga afya bora.

"Nikiwa kama mama wa familia, elimu niliyoipata hapa itanisaidia sana mimi na familia yangu kwa sababu sasa naelewa wakati wa kuandaa chakula niandae chakula gani ambacho kitatusaidia kutujenga kimwili na kutupa afya njema, ikiwemo kula matunda na mbogamboga kwa wingi kwani vinatupatia madini na vitamini kwa wingi mwilini ambayo ndio msingi wa kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali" amesema Shoo.