Halmashauri 14 zapatiwa mafunzo ya kuongeza madini joto

News Image

Imewekwa: 16th Oct, 2018

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imetoa mafunzo ya kuongeza madini joto kwenye chumvi kwa wazalishaji 715 toka halmashauri 14 zinazozalisha chumvi kwa wingi nchini ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Rufiji, Mkuranga, Bagamoyo, Kibiti, Mafia, Meatu, Hanang, Babati, Pangani, Mkinga, Korogwe, Tanga Jiji, Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Kigamboni.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afya na Lishe ya Jamii, Dkt Fatma Abdallah amesema kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wazalishaji wa chumvi nchini ili kuhakikisha chumvi iliyopo sokoni inakuwa imeongezewa madini joto kama ilivyoelekezwa na sheria ya nchi.

Naye Bupe Ntoga, Afisa Utafiti Mwandamizi Lishe amesema kwamba madini joto ni muhimu kwa binadamu toka anapokuwa tumboni, kuzaliwa hadi utu uzima.

“Upungufu wa madini joto kwa mama mjamzito husababisha mtoto kuzaliwa aidha mfu, au kuzaliwa na mtindio wa ubongo pamoja na ulemavu wa viungo vya mwili. Lakini kwa mtu mzima tatizo la upungufu wa madini joto husababisha kuvimba kwa tezi la shingo, kufunga choo, kupungua kwa kasi ya kufikiri na kutenda kazi hali inayoathiri uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla”

Aidha Ntoga amesema kwamba tatizo la upungufu wa madini joto linazuilika kwa mtu kutumia chumvi iliyoongezewa madini joto mara kwa mara, hivyo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha kwamba wananunua na kutumia chumvi iliyoongezewa madini joto.