Zoezi Utafiti gharama za Utapiamlo nchini lazinduliwa rasmi
Imewekwa: 19th Feb, 2024
Februari 14, 2024 Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu imezindua rasmi zoezi la Utafiti kuhusu gharama za Utapiamlo nchini “The Cost of Hunger in Africa-COHA:Tanzania Study” unaolenga kubainisha makadirio ya gharam zinazosababishwa na Changomoto za Lishe duni/ Utapiamlo; Kijamii, Kiuchumi hususani katika Nyanja za sekta ya afya, elimu na uzalishaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kufanyika kwa Utafiti huo utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 22 Barani Afrika kufanya utafiti kama huu na pindi utakapokamilika utaiwezesha nchi kupanga malengo ya kupunguza upotevu wa pato ghafi itokanayo na Utapiamlo na kuwekeza katika maeneo ya Maendeleo.
“Nidhahiri kuwa tafiti hizi zinazofanyika hapa nchini ni moja ya jitihada za kutafuta shahidi za kisayansi zinazoweza kuisaidia Serikali kuboresha harakati zake za kuondokana na athari za Utapiamlo.” Amesema Mhe.Ummy.
Ummy amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia utafiti huu ufanyike nchini na hii inatokana na nia yake ya dhati ya kuondoa Utapiamlo nchini.
Awali akizungumzia kuhusu Utafiti wa Gharama za Utapiamlo unaoenda kufanyika Tanzania Bara na Visiwani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema utafiti huo utasaidia Serikali kuweza kujua hasara kwa upande wa fedha zinazopotea katika vita ya kupambana na Utapiamlo.
Kwa upande Bi.Sarah Gordon- Gibson, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) amesema Tanzania inaenda kuwa miongoni mwa nchi 22 ambazo tayari zimefanya utafiti huo, na Shirika hilo limejitoa kuhakikisha linashirikiana na Serikali kuhakikisha utafiti huo unafanyika kikamilifu na kuweza kutoa ushaidi wa kisayansi utakaosaidia kupambana na tatizo la Utapiamlo
Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais-Zanzibar Salhina Mwita Ameir, amesema tatizo la Utapiamlo ni tatizo ambalo linaendelea kusumbua nchi na watu wake, hivyo ujio wa utafiti huo utaenda kutafuta njia ya kuweza kukabiliana nao.