Dodoma na Singida kupambana na utapiamlo kwa kutumia virutubishi mchanganyiko

News Image

Imewekwa: 3rd Apr, 2019

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Sikitu Simon amesema kwamba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia mradi wa Boresha Lishe limepanga kugawa virutubishi mchanganyiko katika mikoa ya Dodoma na Singida kwa ajili ya kupambana na utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 2.

Ndugu Sikitu amebainisha hayo wakati wa mafunzo ya matumizi ya virutubishi mchanganyiko yanayofanyika kwa siku 3 kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 03/04/2019 katika ukumbi wa Ujenzi jijini Dodoma. Mafunzo hayo yanayotolewa kwa watoa huduma za afya wa mikoa ya Dodoma na Singida yamejumuisha washiriki 38 kutoka katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya za Bahi, Chamwino, Ikungi na Singida Vijijini.

Aidha ndugu Sikitu amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma ili waweze kuwasimamia na kuwaelekeza walengwa juu ya matumizi sahihi ya virutubishi mchanganyiko kwa ajili ya kupambana na utapiamlo.

Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu Sikitu, Tanzania inakabiliwa na aina mbili za utapiamlo ambazo ni utapiamlo wa upungufu wa virutubishi mwilini na utapiamlo wa kuzidi kwa virutubishi mwilini. Aina ya kwanza ya utapiamlo inawakabili zaidi watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano. Waathirika wakuu wa aina ya pili ya utapiamlo ni watu wazima. Utapiamlo unaathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili. Mtoto aliyedumaa kutokana na utapiamlo ana uwezekano mkubwa wa kupata alama za chini za ufaulu shuleni. Pia anakuwa katika uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa sugu yanayohusiana na ulaji wa chakula ikiwemo kisukari, shinikizo kubwa la damu na magonjwa ya moyo. Hivyo wakati sahihi wa kupambana na utapiamlo kwa mtoto ni katika siku 1000 za mwanzo ya maisha yake zinazoanzia tangu mama anapokuwa mjamzito, kujifungua hadi mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.

“Ni muhimu kuhakikisha mama mjamzito anapata matunzo na lishe bora, mtoto anapozaliwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo, na anapotimiza umri wa miezi sita hadi kufikisha miaka miwili apatiwe chakula cha nyongeza kilichoongezewa virutubishi mchanganyiko”.Alisisitiza ndugu Sikitu

Naye Afisa Lishe kutoka Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ndugu Neema Shosho, alieleza kwamba mradi wa Boresha Lishe unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017 katika wilaya nne za mikoa ya Dodoma na Singida ambazo ni Bahi, Chamwino, Ikungi na Singida Vijijini. Kupitia mradi huu wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanapewa kilo 7.5 za unga ulioongezwa virutubishi hususan vitamini na madini muhimu mwilini kwa ajili ya matumizi yao kwa mwezi. Pia watoto wanapewa kilo 6 za unga huo kwa ajili ya matumizi kwa mwezi. Kiasi hiki cha unga ulioboreshwa ni sawa na gramu 250 au robo kilo kwa siku kwa wanawake, na kwa watoto ni sawa na gramu 200 kwa siku. Vyakula hivi hutolewa kwa walengwa kama nyongeza ya mlo wao wa kawaida katika familia.

Pale ambapo vyakula hivyo vinatolewa kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kwa lengo la kutibu utapiamlo, unga wanaopewa huwa umeongezwa virutubishi vingi zaidi ambapo wanapewa kilo 6.9 za unga huo pamoja na mafuta ya kupikia yaliyoongezewa virutubishi.

Mpango huu ulianzishwa na WFP baada ya kufanyika tathimini na kubaini kuwa chakula kinachozalishwa na kaya katika maeneo ya mradi kinakuwa hakina virutubishi vya kutosha. Hata hivyo kwa sasa WFP imeona kwamba njia bora ni kuwapatia walengwa virutubishi mchanganyiko ambavyo watavitumia kuongeza kwenye chakula cha mtoto mwenye umri chini ya miaka miwili.

“Kwa hiyo sasa tunabadilisha utaratibu, hatutakuwa tunagawa tena unga kama awali kwa kipindi chote cha mwaka mzima bali tutakuwa tunagawa katika kipindi cha mahitaji hasa wakati wakiangazi kuanziamwezi Oktoba hadi mwezi Machi” Alisema ndugu Neema Shosho.