DKT. YONAZI: TUIMARISHE LISHE, TUPUNGUZE MAGONJWA SUGU

Imewekwa: 30th Sep, 2025
NA. MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wadau kushirikiana na Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini ili kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Amesema ulaji usiofaa na mitindo mibaya ya maisha vimechangia kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza jambo linalohatarisha maendeleo ya Taifa.
Dkt. Yonazi ameyasema hayo jijini Dar es salaam leo 29 Septemba, 2025 katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Wadau wa Lishe nchini unaoendelea katika kituo cha mikutano cha APC Bunju jijini Dar es Slaam.
Dkt. Yonazi amesema tafiti zinaonesha kuwa uzito uliozidi na uliokithiri ni chanzo kikuu cha magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yakiwemo kisukari, moyo, figo na baadhi ya saratani.
“Napenda kukumbusha wadau, taasisi na wataalam kushirikiana na serikali kufanya tafiti zitakazosaidia kuleta majibu ya changamoto za lishe, pamoja na kusaidia watu kubadili tabia za ulaji na mtindo wa maisha ili kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza yanayohusiana na ulaji usiofaa na ambayo ni tishio kwa Taifa letu,”alisema Dkt. Yonazi.
Dkt.Yonazi ameongeza kuwa Takwimu zinaonesha licha ya hali ya lishe nchini kuendelea kuimarika bado kuna changamoto hususani kwenye uzito uliozidi na kiriba tumbo hii kutokana maendeleo tunayoyapata na mabadiliko ya mtindo wa maisha hususani ulaji usiofaa hivyo jitihada za pamoja kati ya wadau na serikali zinahitajika ili kukabiliana na tatizo hili.
Akizungumza kuhusu mkutano huo Dkt. Yonazi amesema lengo ni kupokea na kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Mwaka wa Tatu 2024/2025 katika maeneo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe (2021/22-2025/26).
Vilevile amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau wote wa lishe kujadili namna utekelezaji ulivyofanyika, changamoto na mikakati ya kufanikisha utekelezaji katika kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa mpango huo hususan mwaka 2025/26.