Naibu Waziri azindua Bodi ya TFNC na kutoa maagizo

News Image

Imewekwa: 17th Jan, 2019

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) ameagizaBodi ya Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) kupambana na utapiamlo kwa kuwekeza katika lishe ili watanzania wengi wasipate magonjwa, wakati akiizindua rasmi bodi hiyo tarehe 18 Disemba, 2018.

Akitoa maagizo hayo Dkt. Ndugulile amesema kwamba Taasisi ina jukumu kubwa kuhakikisha inapambana na aina zote za utapiamlo

“Licha ya juhudi zilizofanyika Tanzania bado inakabiliwa na tatizo la udumavu. Mbali nahilo kuna tatizo zaidi la lishe iliyopitiliza ambalo husababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na baadhi ya saratani. Matatizo haya mawili ni changamoto ambapo ni gharama kubwa kwa Serikali, kwa mfano kupandikiza figo kwa mgonjwa mmoja nchini India Serikali inatumia zaidi ya milioni 100 na akifanyiwa hapa nchini ni shilingi milioni 20”

Kwa kutambua hilo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akatoa maagizo yafutayo:

Elimu ya Lishe, amesema kuwa wananchi wengi hawana elimu ya lishe licha ya kuwa upatikanaji wa chakula sio tatizo, hivyo wananchi waelimishwe juu ya ulaji unaofaa kwa kutumia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari, mitandao ya kijamii. Pia alihimiza Taasisi kushirikiana na kitengo cha elimu ya afya kwa umma kilichopo chini ya Wizara ya Afya.

Aidha alishauri elimu ya lishe iingizwe kwenye mitaala ya elimu kuanzia shule za msingi.

Tafiti za Lishe, Taasisi imeagizwa kufanya na kusimamia tafiti zinazotoa majibu kuhusu matatizo ya lishe kama vile udumavu, utunzaji wa vyakula, sumu kuvu n.k

Ubunifu kazini, ameiagiza bodi kuisimamia menejimenti ipasavyo kuhakikisha inafanya kazi kwa ubunifu kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuendeleza taasisi ikiwemo rasilimali watu yenye elimu ya juu mathalani watumishi wenye shahada za uzamivu (PhD) na akahoji kwa kiasi gani wametumika kuandika maandiko ili kuleta fedha katika taasisi. Pia, ametaja mifano ya rasilimali nyingine zinazo milikiwa na taasisi ambazo zikisimamiwa vizuri zitaleta manufaa makubwa ikiwemo maabara na kitengo cha uchapishaji.

Sheria, aidha ameagiza kufanyika kwa mapitio ya sheria iliyoanzisha Taasisi (Sheria ya Bunge Na. 24 ya 1973) ili kujibu changamoto za lishe zilizopo sasa kwani sheria hiyo ni ya muda mrefu na ilipitiwa kwa mara ya mwisho mwaka 1995.

Utumishi, Bodi pia imeagizwa kuhakikisha inapata wakurugenzi wa kudumu kwani waliopo sasa wanakaimu nafasi hizo.

Muundo wa Taasisi, pia imeagizwa kupitia muundo huo ili unaendana na mahitaji ya sasa, kwani muundo huo ni wa muda mrefu.

Ushirikiano Kazini, Dkt Ndugulile amaitaka bodi kuhakikisha inaweka na kuendeleza mazingira safi ya kuhakikisha menejimenti na watumishi wa Taasisi wanafanya kazi kwa ushirikiano bila ya kuwa na makundi kwani makundi yanazorotesha utendaji wa kazi.

Kutumia viongozi wastaafu, aidha ameishauri bodi kutumia watalaamu wa ndani ya nchi hususan wakurugenzi watendaji waliowahi kuongoza taasisi hiyo ambao ni hazina kubwa katika kuishauri taasisi kuliko kutegemea zaidi watalaamu wa kigeni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Joyce Kinabo alitoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteu kuwa mwenyekiti, pia alimshukuru Waziri wa Afya kwa kuwateua wajumbe nane wa bodi na akaahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa.

Aidha baada ya ufunguzi, bodi ilikutana na menejimenti na watumishi wa TFNC kwa lengo la kujitambulisha na kutoa maelekezo kwa ajili ya utekelezaji.

Bodi ya Taasisi inaongozwa na Prof. Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na wajumbe nane ambao ni Ombaeli Lemweli (Wizara ya Kilimo na Usalama wa Chakula), Lora Madete (Wizara ya Fedha na Mipango), Mwita Waibe (OR TAMISEMI) and Jamal Kusaga (SUA). Wengine ni Pazi Mwinyimvua (UDSM), Leonard Subi (Wizara ya Afya), Mwajuma Magwiza (Wizara ya Afya) and Theresia Kuiwite (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia).