Ushauri kuhusu ulaji wa chakula kwa wagonjwa wa kisukari

Matibabu ya ugonjwa wa kisukari yanagharimu fedha nyingi. Kwa hiyo ni muhimu kuzuia na kudhibiti athari za kisukari mapema. Ili kudhibiti ugonjwa wa kisukari mgonjwa anapaswa kupatiwa matibabu sahihi, kufuatilia na kupima hali yake ya afya mara kwa mara pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha na taratibu zinazofaa za ulaji wa chakula.

Zifuatazo ni kanuni za ulaji unaofaa zinazopaswa kuzingatiwa na mgonjwa wa kisukari:

1.Kula mlo kamili (angalau mara 3 kwa siku) kwa kuzingatia muda mahususi aliojipangia kwani hashauriwi kukaa na njaa kwa muda mrefu.

2.Dhibiti kiasi cha nishati – lishe (wanga) katika chakula ili kisizidi mahitaji ya mwili. Kiasi kitegemee mahitaji ya mtu binafsi.

3.Ongeza ulaji wa vyakula vyenye makapi – mlo kwa wingi. Kiasi kikubwa cha nishati-lishe kitokane na vyakula vya asili ya nafaka isiyokobolewa, mizizi na ndizi za kupika. Sukari inayotoka katika vyakula hivi hufyonzwa kwa taratibu na hivyo kupunguza kasi ya ongezeko la sukari katika damu.

4.Punguza kiasi cha vyakula vinavyozalisha nishati lishe kwa wingi hususani vyakula vyenye mafuta kwa wingi.

5.Panga utaratibu wa kula chakula na matumizi ya dawa. Iwapo unatumia insulin au dawa za kushusha kiwango cha sukari katika damu unapaswa kujipangia muda wa kula chakula na kumeza dawa ili kuzuia kupungua kwa sukari katika damu. Epuka kukaa kwa muda mrefu bila kula chakula.

6.Kula mbogamboga kwa wingi katika kila mlo.

7.Kula tunda katika kila mlo.

8.Epuka kunywa pombe.

9.Epuka ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, keki, biskuti, pipi na asali.

Kanuni nyingine za kuzingatia ni:

1.Punguza uzito iwapo una uzito uliozidi - au dhibiti uzito wa mwili ili usifikie uzito uliozidi. Ni muhimu kuwa na uwiano sahihi wa uzito wa mwili kulingana na urefu wako.

2.Zingatia usafi na usalama wa chakula