Lishe ya Mama anayenyonyesha

Mama anayenyonyesha anatakiwa kuwa na lishe bora kutokana na kuwa na mahitaji makubwa ya virutubishi mwilini kwa ajili ya afya yake na kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto. Kwa sababu hiyo, ni muhimu mama anayenyonyesha kula mlo kamili zaidi ya mitatu kwa siku na asusa kati ya mlo na mlo.

Umuhimu wa ulaji unaofaa kwa mama anayenyonyesha

Lishe bora kwa mama anayenyonyesha ni muhimu ili:

  • Kuwa na afya bora kwani humpatia virutubishi vya kutosha kutokana na ongezeko la mahitaji ya virutubishi wakati wa unyonyeshaji
  • Kuhuwezesha mwili wake kutengeneza na kutoa maziwa ya kutosha kadri mtoto anavyohitaji.
  • Kuimarisha kingamwili za mama zidi ya maradhi mbalimbali
  • Kuzuia upungufu wa damu kwa mama na mtoto, lishe bora huongeza akiba ya madini chuma ambayo hutumika kwa mama na kwa mtoto kupitia maziwa ya mama.
  • Kumwezesha mtoto kuwa na afya bora kutokana na kupata maziwa ya kutosha kutoka kwa mama

Mambo muhimu ya kuzingatia

Ili kuboresha hali yake ya lishe kwa mama anayenyonyesha, anashauriwa kuzingatia mambo yafuatayo:

  • Kula milo kamili zaidi ya mitatu kwa siku, mlo kamili ni mlo wenye chakula mchanganyiko angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la chakula.
  • Kula chakula kingi na cha kutoshakatika kila mlo.
  • Kula asusa kati ya mlo na mlo.
  • Kumeza vidonge vya kuongeza damu (FEFO) kwa kipindi cha miezi 3 baada ya kujifungua.
  • Kutumia vyakula vilivyoongezwa virutibishi, kama vile unga wa ngano, unga wa mahindi, mafuta ya kupikia na kutumia chumvi yenye madini joto.
  • Kuongeza ulaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama mfano nyama, kuku, mayai, maziwa, samaki, dagaa n.k. Vyakula vya asili ya wanyama vina virutubishi vya aina mbalimbali kwa wingi ikiwemo madini chumaambayo husaidia kuongeza damu mwilini.
  • Kutumia chumvi yenye madini joto
  • Kula matunda ya aina mbali mbali na mbogamboga kwa wingi
  • Kunywa maji ya kutosha kila siku (angalau glasi 8 au lita 1.5),.
  • Kujikinga na Malaria kwa kulala kwenye vyandarua vilivyowekwa dawa kila siku.
  • Kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na virusi vya UKIMWI

Kumbuka:

Mama anayenyonyesha ni muhimu kusaidiwa kazi nzito ili apate muda wa kutosha wa kupumzika na kumnyonyesha mtoto mara kwa mara kila anapohitaji, usiku na mchana.