Dondoo muhimu kuhusu mtindo bora wa maisha ili kuzuia na kukabiliana na saratani.

Saratani na matibabu yake huweza kumfanya mtu kuwa dhaifu. Ni muhimu sana kwa mgonjwa wa saratani kuzingatia ulaji bora na kufuata mtindo bora wa maisha kwa sababu unasaidia sana kupunguza madhara ya ugonjwa kabla, wakati na baada ya tiba. Hata kwa wale waliugua na kupona saratani wanahitaji kudumisha mtindo bora wa maisha ili kupunguza uwezakano wa saratani kurudi tena.

Hivyo ni muhimu kila mmoja kuzingatia ushauri ufuatao:

Tumia vyakula vitokanavyo na mimea Zaidi:

 • Kula mboga-mboga na matunda kwa wingi kila siku.
 • Kula mboga-mboga za kijani, njano, nyekundu, zamabarau na rangi nyingine zilizopikwa angalau ujazo wa kikombe kimoja katika kila mlo. Tumia pia mboga zisizopikwa, kama vile saladi, nyanya, matango n.k; hakikisha mboga-mboga zinazoliwa mbichi zinaoshwa vizuri kwa maji safi na salama.
 • Kula matunda ya aina mbalimbali angalau tunda moja katika kila mlo. Kumbuka matunda halisi ni bora kuliko juisi .
 • Kumbuka mchanganyiko wa mboga-mboga au matunda yenye rangi mbalimbali huongeza ubora wake.
 • Hakikisha katika kila mlo unatumia nafaka zisizokobolewa kama vile unga wa mahindi wa dona, mchele wa blauni (usiong’arishwa), unga wa ngano usiokobolewa/usiong’arishwa au ngano isiyosagwa, pia ulezi, mtama au uwele kwani havikobolewi; na
 • Tumia vyakula mbalimbali vya jamii ya kunde kama vile maharagwe, kunde, njegere kavu, njugu mawe, dengu, choroko na mbaazi.

Punguza matumizi ya nyama nyekundu.

 • Kwa wale wanaotumia nyama nyekundu, ni muhimu kuitumia kwa kiasi, isizidi nusu kilo kwa wiki. Nyama nyekundu ni pamoja na ile ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe. Ni vyema kutumia nyama nyeupe kama samaki au kuku.

Epuka matumizi ya nyama zilizosindikwa.

 • Nyama zilizosindikwa ni pamoja na zile zilizohifadhiwa kwa kuongezwa chumvi, mafuta, kemikali au kukaushwa kwa moshi. Nyama hizi zimeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani. Nyama hizo ni paomoja na nyama za makopo, soseji (hotdogs), bekoni (bacon) n.k.

Kuwa na uzito wa mwili wa wastani.

 • Uzito wamwili uliozidi kiasi sio tu huchangia kuongeza uwezekano wa kupata saratani, bali pia huongeza hatari ya uvimbe wa saratani kurudi hata pale ambapo ulishatolewa. Unene uliozidi kiasi pia huongeza uwezekano wa kupata maradhi mengine sugu. Ni muhimu kuwa na uzito wa wastani lakini pia usipungue kuliko invyotakiwa. Kwa mtu mzima ni vizuri kuwa na uzito wenye uwiano wa uzito na urefu (BMI) kati ya 21 na 2. (Pata ushauri Zaidi kuhusu BMI kutoka kwa mtaalamu wa afya/lishe).
 • Punguza ulaji wa vyakula vinavyochangia ongezeko la uzito wa mwili kwa haraka hasa vile vyenye mafuta mengi au sukari nyingi.
 • Mafuta yatumike kwa kiasi kidogo. Mafuta huupatia mwili nishati-lishe na pia husaidia utumikaji mzuri wa baadhi ya virutibishi mwilini, lakini huhitaji kwa kiasi kidogo. Epuka vyakula vyenye mafuta mengi. Vyakula hivyo ni pamoja na vile vinavyopikwa kwa kudumbukizwa kwenye mafuta au kukaangwa kwa mafuta mengi. Vyakula hivyo ni kama chips, vitumbua, maandazi, sambusa, chapati nk. Vyakula hivi ni bora kuviepuka au viliwe mara chache na kwa kiasi kidogo sana.
 • Epuka matumizi ya vinywaji, asusa au vyakula vyenye sukari nyingi kama soda, juisi bandia (vinywaji hivi ni mchanganyiko wa maji, rangi, sukari na ladha bandia), chokoleti, keki, ice-cream nk.
 • Kama unaongezeka uzito kuliko kawaida, epuka ulaji wa asusa (vitafunwa) zenye nishati-lishe nyingi kati ya mlo na mlo na badala yake ongeza vyakula vyenye makapi-mlo kwa wingi kama matunda, mboga-mboga na nafaka zisizokobolewa/zisizong’arishwa.

Punguza matumizi ya chumvi.

 • Kwa wastani mwanadamu anahitaji gramu 6 za chumvi kwa siku (sawa na kijiko cha chai kilichojazwa kwa usawa wa bapa au mfuto). Lakini tukumbuke vyakula vingi tayari vina chumvi kwa asili. Ni bora kuongeza ladha kwenye chakulakwa kutumia viungo mbalimbali badala ya chumvi.
 • Epuka vyakula vilivyosindikwa kwa kuongeza chumvi na vyakula vilivyoongezwa chumvi nyingi.
 • Usiongeze chumvi kwenye chakula wakati wa kula.

Epuka vyakula vilivyoota fangasi au ukungu.

 • Vyakula vya aina ya nafaka, jamii ya kunde, karanga au korosho huota ukungu iwapo havikuhifadhiwa vizuri. Ukungu huu husababishwa na fangasi ambazo hutoa sumu iitwayo sumu kuvu “aflatoxin”. Sumu hii ina hatarisha afya na pia huweza kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani.

Epuka utumiaji wa tumbaku au sigara.

 • Utumiaji wa tumbaku ikiwa ni pamoja na uvutaji sigara umeonekana kusababisha baadhi ya saratani, hasa zile za mapafu.
 • Uvutaji wa sigara pia huingilia na kudhoofisha mfumo wa kinga hivyo kuongeza uwezakano wa kupata baadhi ya saratani.

Epuka matumizi ya pombe.

 • Pombe imeonekana kuongeza uwezekano wa kupata aina nyingi za saratani hasa zile za mdomo, koo, matiti na tumbo. Hivyo kutokana na uhusiano wake na saratani, inashauriwa kuepuka pombe sio tu katika kuzuia bali pia kupunguza uwezekano wa hali ya afya ya mtu mwenye saratani kuwa mbaya Zaidi.
 • Pombe huweza kuingilia umeng’enyaji wa chakula na ufyonzaji wa virutubishi mwilini, na pia huingilia uhifadhi wa baadhi ya vitamini na madini mwilini.

Fanya mazoezi ya mwili.

 • Kufanya mazoezi ya mwili kila siku kumeonekana kuzuia saratani za aina nyingi. Kutofanya mazoezi ya mwili kumeonekana kuongeza uwezekano wa kupata saratani na pia kuchangia ongezeko la uzito wa mwili. Mazoezi ni paomoja na kutembea, kufanya kazi za nyumbani kama vile bustani, kufua, kufanya usafi n.k.
 • Fanya mazoezi kila siku kuufanya mwili kuwa mkakamavu pamoja na kusaidia chakula kuyeyushwa na kufanya kazi vizuri.
 • Anza kwa kufanya mazoezi ya mwili ya wastani kama vile kutembea harakaharaka angalau dakika 30 kila siku na mwili ukishazoea, ongeza hadi kufikia dakika 60 kila siku. Kama unafanya mazoezi ya nguvu sana, basi iwe angalau dakika 30 kila siku.
 • Punguza sana mtindo wa maisha ambao unakufanya uketi bila mazoezi kama vile kuangalia televisheni kwa muda mrefu au kufanya kazi ukiwa umeketi kwa muda mrefu.
 • Kwenye jengo la gorofa tumia ngazi badala ya lifti.

Epuka kutumia virutubishi vya nyongeza (supplements) kwa nia ya kuzuia saratani.

 • Virutubishi vya nyongeza havizuii saratani na kuna aina nyingine ya virutubishi vinapotumika kama nyongeza huchangia kuongeza uwezekano wa kupata saratani. Ni vyema kupata mahitaji yako ya virutubishi kutokana na kula vyakula vya mchanganyiko. Muone daktari kwa ushauri kabla ya kutumia virutubishi vya nyongeza au unapodhani una upungufu wa virutubishi.

Mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama.

 • Unyonyeshaji wa maziwa ya mama umeonekana kupunguza uwezekano wa kupata saratani kwa mama na mto. Inashauriwa mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila kitu kingine chochote (hata maji) katika miezi sita ya mwanzo. Baada ya miezi sita aendelee kunyonyeshwa na kupewa chakula cha nyongeza hadi atimize miaka miwili au Zaidi.

Mambo mengine yanayoweza kumsaidia mgonjwa wa saratani ni:

 • Kunywa maji ya kutosha ili kumaliza kiu.
 • Kunywa angalau glasi nane kwa siku
 • Maji ya madadu na togwa pia ni vinywaji vizuri iwapo vinapatikana.
 • Inapowezekana tumia maziwa ya mgando (mtindi). Maziwa ya mgando huyeyushwa kwa urahisi pia husaidia ufyonzwaji wa virutubishi tumboni kutoka kwene vyakula vingine.
 • Kama inawezekana, tumia mafuta ya zeituni kidogo kama sehemu ya mlo.
 • Ongeza matumizi ya viungo mbalimbali kama vile vitunguu saumu, majani mbalimbali ya viungo, binzari halisi, n.k.

Muhumu:

Ni muhimu kupata ushauri wa daktari pale ambapo aina ya matibabu inaweza kuhitaji mabadiliko katika ulaji.