Wenye kifua kikuu na VVU kupata elimu ya lishe kiganjani

News Image

Imewekwa: 6th Mar, 2023

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamezindua Programu ya Simu inayohusu Masuala ya Lishe kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI pamoja na kifua kikuu ili kusaidia kukabiliana na magonjwa nyemelezi na kuimarisha hali zao za lishe.

Akizundua Programu hiyo Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu amesema programu hiyo itaongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na magonjwa hayo na ikiwezekana kuyatokomeza kabisa.

Programu hiyo kwa sasa itapatikana kwenye simu zenye mfumo wa Android na baadae kwenye simu zenye mfumo wa IOS na ambayo itamuwezesha mgonjwa wa kifua kikuu na mtu anayeishi na ugonjwa wa UKIMWI kumwezesha kupata elimu ya mlo kamili kupitia video na majarida mbalimbali pamoja kujifanyia tathmini ya hali yake la lishe.

"Lishe hii ni moja ya mikakati ya kuwajengea wananchi uelewa kuhusu masuala ya lishe bora na kuchochea mfumo bora wa lishe,kupitia programu hii naamini itasaidia kutoa elimu na ujuzi namna ya kuandaa milo na kutumia vyakula vinavyopatikana katika maeneo husika,

Hii itasaidia kufikia malengo ya wizara ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza,"amesema Prof Nagu.

Ili kufanikisha malengo ya Serikali, Profesa Nagu ameitaka TFNC kuhakikisha kupitia Programu hiyo inawafikia watu wengi zaidi wakiwamo wenye magonjwa ya Kisukari na Saratani

Makundi mengine aliyoagiza Profesa Nagu yafikiwe ni watoto wadogo, wachanga,vijana balehe; wajawazito na wanawake wanaonyonyesha pamoja na; makundi mengine ili kuongeza chachu ya mabadiliko chanya katika ulaji unaofaa na mitindo bora wa maisha.

Pia ameiagiza Taasisi hiyo kubuni njia za kuwafikia wanaume ili kuleta uelewa wa pamoja katika familia kwa lengo la kukinga badala ya kutibu.

"Wekeni huduma itakayomsaidia mtumiaji kufanya tathimini ya kiasi ya chakula alichokula na mpangilio wa mlo kama unatimiza vigezo vinavyotakiwa kulingana na shughuli anayoifanya,"amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzaniaa, Dkt. Germana Leyna amesema mwaka 2020 walifanya tathmini katika mkoa wa Geita na Singida kuangalia hali za lishe na uelewa wa huduma za afya kwa watu wenye VVU na kubaini kundi hilo lina uelewa mdogo.

Amesema katika mahojiano yao ya ana kwa ana na watu wenye VVU takribani 20 na kubaini 18 hawana uelewa wa masuala ya lishe.

"Walikuwa hawana taarifa kamili japo namba ya idadi ni ndogo lakini kwetu ilikuwa inaonekana elimu hii haijawafikia watu kwenye vituo vya afya japo watoa huduma wapo,

Tunajua kuna changamoto labda wanazidiwa na kazi au muda sio rafiki lakini tuliona kwamba bado wanahitaji elimu, kwa hiyo ilikuwa elimu hiyo tuitoeje ili kufikia watu wengi zaidi, ndipo wazo la kutumia App ya kiganjani ilipokuja,"amesema Dkt. Germana Leyna.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Bi.Sarah Gordon-Gibson amesema wataendelea kuwekeza kwenye lishe na kuendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe katika kukabiliana na afua mbalimbali za lishe ikiwemo zile ambazo zinaelekezwa kwenye Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bw.Obey Assey amesema haya ni mapinduzi makubwa ambayo yamefanyika kwenye Masuala ya lishe na kupitia programu hiyo itaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuitaka Menejimenti ya Taasisi kuhakikisha wanaisimamia programu hiyo na hata iweze kutumika kuwafikia makundi mengine.