Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani mwaka 2018

News Image

Imewekwa: 19th Jun, 2018


KAULI MBIU: “Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama ni Msingi wa Maisha”

1.0 Utangulizi

Kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti, Tanzania huungana na nchi nyingine kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani. Maadhimisho hayo yana lengo la kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama na pia kuweka msukumo wa kipekee katika kuunganisha nguvu ya wadau mbalimbali ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Maadhimisho hayo huambatana na kauli mbiu maalum zinazolenga kuhamasisha na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto na taratibu sahihi za ulishaji watoto wachanga na wadogo. Hii husaidia kukabiliana na tatizo la utapiamlo nchini na hasa udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano. Kauli mbiu ya mwaka huu 2018 ni: Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama ni Msingi wa Maisha”. Pia maadhimisho haya hutoa fursa nzuri kwa viongozi wa ngazi mbalimbali kutoa uamuzi na kulipa kipaumbele suala zima la unyonyeshaji na hivyo kulifanya ni ajenda katika mikutano mbalimbali na kutenga raslimali fedha ili kuweza kutekeleza afua zinazohusu ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni fursa muhimu ya kutoa hamasa kwa jamii katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji. Unyonyeshaji ni suluhisho ambalo linampa kila mtu msingi imara wa mwanzo wa maisha. Husaidia katika kuboresha afya na ustawi wa wanawake na watoto duniani kote.

1.2 MALENGO YA WIKI YA UNYONYESHAJI DUNIANI 2018

Mwaka huu 2018 malengo ya unyonyeshaji ni:

  • Kuitaarifu jamii kuhusu uhusiano uliopo kati ya lishe bora, uhakika wa chakula, kupunguza umasikini na unyonyeshaji.
  • Kusisitiza unyonyeshaji ni msingi wa maisha
  • Kushirikisha watu binafsi, asasi za kiraia ili kuleta matokeo mazuri
  • Kuimarisha hatua za kuhamasisha unyonyeshaji kwa lengo la kujenga jamii yenye lishe bora, uhakika wa chakula na kupunguza umasikini.

1.3 Kauli mbiu ya Wiki ya Unyonyeshaji kwa mwaka 2018

Kauli mbiu ya mwaka huu inasisitiza umuhimu wa maziwa ya mama kwa afya na uhai wa mama na mtoto. Inashauriwa kuwa mama anyonyeshe mtoto wake maziwa yake pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, na apewe chakula cha nyongeza anapotimiza miezi sita, huku akiendelea kunyonyeshwa hadi kufikia miaka miwili au zaidi.Hivyo basi, ni muhimu kwa mama kupata msaada katika jamii husika kwa wakati na pamoja na kupata elimu ya afya na unyonyeshaji unaofaa kutoka katika vituo vinavyotoa huduma ya afya.

Uyonyesha ni jukumu la kila mtu katika nafasi yake, wadau hao ni pamoja na familia, viongozi ngazi ya jamii, wafanyakazi wa afya wenye ujuzi, wataalamu wa masuala ya unyonyeshaji na marafiki. Ni vizuri kwa mama kupata muda na msaada wa kutosha katika kipindi cha kunyonyesha na pia apate elimu ya makuzi na malezi kwa mtoto wake. Hivyo basi ili kuufanya unyonyeshaji uwe endelevu mama anahitaji msaada toka kwa kila mwana jamii na hasa mama apate unasihi wa maswala ya unyonyeshaji toka kwa mhudumu wa afya ya jamii kuweza kumsaidia kutatua changamoto za ulishaji wa mtoto wake.

1.4 Kwa nini tunaadhimisha wiki ya Unyonyeshaji?

Takwimu kutoka maeneo yote duniani zinaonesha kuwa kiwango cha watoto wanaoanzishiwa kunyonya maziwa ya mama kwa wakati sahihi ni vya kuridhisha, ni asilimia 40 tu ya watoto wote wenye umri chini ya miezi sita hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji au vyakula vingine, na ni asilimia 45 tu huendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi wanapofikisha umri wa miaka miwili. Zaidi ya hayo, kuna tofauti kubwa za takwimu za unyonyeshaji kikanda pia kati ya nchi moja na nyingine na hata kati ya mkoa mmoja na mwingine ndani ya nchi. Tunapotoa msukumo katika unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa kufuata taratibu sahihi huzuia vifo vya watoto zaidi ya wapatao 823 000 na vifo 20 000 vya wanawake vinavyotokana na uzazi kila mwaka. Pia, kutonyonyesha watoto maziwa ya mama kunapunguza uwezo wa kiakili wa watoto na kusababisha hasara kiuchumi ambapo dunia hupoteza takribani dola za kimarekani 302 bilioni kila mwaka.

Tanzania imefanya juhudi kubwa katika Ulishaji wa watoto wachanga na wadogo, lakini mpaka sasa hali hairidhishi kama takwimu za mwaka 2015/16 zinavyoonyesha. Utafiti wa Hali ya Afya na Demografia wa mwaka 2015/16 unaonyesha kuwa katika kila wanawake 10 wanaonyonyesha 9 wananyonyesha watoto wao, lakini unyonyeshaji huo haufanyiki kama inavyostahili. Wanawake 5 tu kati ya 10 wanaojifungua hunyonyesha watoto wao katika saa moja ya mwanzo na wanawake 6 kati ya 10 huendelea kunyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo.

Hata hivyo utafiti huo unaonyesha kuwa watoto 4 kati ya 10 wenye umri chini ya miezi sita hupewa vinywaji au vyakula vingine mbali na maziwa ya mama. Watoto 3 kati ya hao (10) hupewa vinywaji kwa kutumia chupa za kulishia watoto.Takwimu pia zinaonyesha kuwa ni asilimia 8 tu ya watoto walio katika umri wa miezi 6-23 hupewa vyakula vya nyongeza kwa kuzingatia vigezo muhimu vya umri, kiasi, idadi ya milo kwa siku, uzito na ulaini wa chakula na mchanganyiko wa vyakula mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula cha asili ya wanyama. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya watoto wenye umri kati ya miezi 6-8 wanakuwa wamepata vyakula vya nyongeza na asilimia 97 ni kwa watoto wenye umri kati ya miezi 9-11.

Ni ukweli usiopingika kuwa Maziwa ya mama ni chakula maalumu ambacho kimetengenezwa kukidhi mahitaji ya lishe na kingamwili kwa mtoto. Unyonyeshaji ni njia asilia ya ulishaji watoto na huimarisha uhusiano baina ya mama na mtoto, katika mazingira na hali yeyote ya kiuchumi na kijamii.

Kuna vikwazo vingi vinavyoathiri mazingira yanayowezesha wanawake kunyonyesha watoto wao. Baadhi ya vikwazo hivyo ni pamoja na kuwa na huduma hafifu za afya na lishe hususani katika ngazi ya jamii, wanawake wanaonyonyesha kukosa msaada katika ngazi ya familia, jamii na mahala pa kazi, na hata baadhi ya waajiri kutokutekeleza sera za kazi zinazolenga kuwawezesha wanawake kuwanyonyesha na kuwalisha watoto wao. Sababu nyingine ni wafanyabiashara wa maziwa mbadala, vyakula vya watoto wachanga na wadogo na bidhaa zinazoambatana navyo kutozingatiaKanuni zinazosimamia Usambazaji na Uuzaji wa vyakula hivyo katika nchi yetu.

Kutokana na changamoto hizi, juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza kufikia lengo la Baraza la Afya Duniani. Lengo hilo ni kufikia angalao asilimia 50 ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji au vyakula vingine ifikapo mwaka 2025.

Ingawa tumeweza kupiga hatua katika kuboresha viwango vya unyonyeshaji, bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuondoa mapungufu yaliyopo kati sera na mikakati ya utekelezaji. Sote tunapaswa kuhamasisha unyonyeshaji ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa kuboresha lishe ya jamii, kuimarisha uhakika wa chakula na kupunguza umasikini.

Maelezo zaidi: Bonyeza Hapa WBW 2018