Ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile (Mb)

News Image

Imewekwa: 27th Sep, 2018

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile (Mb) siku ya Jumanne tarehe 25 Septemba, 2018 alifanya ziara ya kikazi katika Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri alianza kwa kutembelea maabara ya Taasisi iliyopo eneo la Mikocheni B Jijini Dar Es Salaam ili kukagua hali ya utendaji kazi katika maabara hiyo. Baada ya hapo alifanya mazungumzo na Menejimenti ya Taasisi kujadili masuala ya kiuongozi; ikiwa ni pamoja na changamoto zinazoikabili Taasisi hivi sasa. Baada ya hapo, Mheshimiwa Naibu Waziri alipokea taarifa fupi ya utendaji wa Taasisi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi, Dkt. Vincent Didas Assey.

Aidha, Mheshimiwa Naibu Waziri alipokea risala ya Wafanyakazi wa Taasisi kutoka kwa Bibi Odina Sansoka Kalinga, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Tawi la Taasisi (RAAWU). Mhe. Naibu Waziri alikamilisha ziara yake kwa kuzungumza na Jumuiya ya Wafanyakazi wa Taasisi.

Katika hotuba yake; pamoja na kutoa maagizo mbalimabli, Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa rai kwa Uongozi wa Taasisi na wafanyakazi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuongeza ubunifu katika kazi, kuimarisha huduma za utoaji elimu kwa umma, hususan umuhimu wa lishe bora katika siku 1000 za kwanza za uhai wa mtoto. Vile vile, Mheshimiwa Naibu Waziri alisisitiza Taasisi kutoa elimu kwa umma kuhusu uhusiano wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, mfano kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya moyo na maradhi mengine kama saratani, n.k. yanayosababishwa na ulaji duni na mitindo isiyofaa ya maisha, ikiwa ni pamoja na unywaji wa pombe uliopitiliza, matumizi ya tumbaku na kutofanya mazoezi ya mwili. Magonjwa haya yameendelea kuongezeka na kuathiri jamii zetu na kuwa mzigo mkubwa kwa familia, jamii na Serikali kutokana na gharama za matibabu yake kuwa kubwa na hudumu kwa maisha yote hivyo huathiri nguvu kazi ya Taifa.

Mwisho, Mheshimiwa Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa Taasisi kujitangaza zaidi na kujiimarisha kimapato kupitia uandaaji wa Kanuni za Sheria Na. 24 ya mwaka 1973 iliyoanzisha Taasisi. Naibu Waziri alikamilisha mazungumzo yake kwa kusisitiza kuwa Serikali inatambua kuwa lishe bora kwa watoto na kwa watu wote ni msingi madhubuti wa kizazi chenye uwezo wa kubuni na kutekeleza kwa vitendo ili kufikia Tanzania yenye maendeleo endelevu ya uchumi wa viwanda.