29 Jan, 2026
Wizara ya Afya, Wizara ya Viwanda na Biashara, Tasisisi ya Chakula na Lishe Tanzania, na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa uratibu wa Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula nchini (TFFA), wanatarajia kufanya utafiti wa kwanza wa kitaifa nchini tangu kuanza kwa afua ya urutubishaji utakaowezesha kutazama ubora, usalama na upatikanaji wa malighafi za virutubishi zinazoingizwa na kuzalishwa nchini na kutumika kwenye urutubishaji wa vyakula hususani unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kupikia pamoja na Chumvi.
Leo Januari 29 Baadhi ya Watalaamu kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Viwanda na Biashara, Tasisisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye Vyakula (TFFA), wamekutana katika ofisi za TFNC zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na kujadili maandalizi ya utafiti huo ambao umefadhiliwa na Shirika la GAIN na TechnoServe Tanzania.
Mwenyekiti mwenza jukwaa la urutubishaji nchini Bw. Gwao Omari Gwao amesema, Utafiti huo utafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Singida, Dodoma, Songwe, Rukwa, Mbeya, Kigoma na Katavi na unatarajiwa kutoa mwongozo muhimu katika kusaidia kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ubora na usalama wa virutubishi (micronutrients) vinavyopatikana nchini na litaangazia Virutubishi vyote vilivyoidhinishwa kisheria kwa ajili ya kurutubisha unga wa Mahindi, ngano, mafuta ya kupikia na chumvi.
