TFNC na wadau wa lishe nchini mbioni kukamilisha program ya kitaifa ya urutubishaji wa vyakula
13 Mar, 2026
TFNC na wadau wa lishe nchini mbioni kukamilisha program ya kitaifa ya urutubishaji wa vyakula
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Wadau wengine wa urutubishaji kupitia ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wako mbioni kukamilisha program ya kitaifa ya urutubishaji wa vyakula ikiwemo uwekaji wa madini joto kwenye chumvi. Kukamilika kwa mpango huo kunatajwa kutasaidia kuhakikisha suala la uongezaji wa viritubishi kwenye vyakula linafanyika kwa upana zaidi ili kuwafikia watu wengi na utaenda kuwaelekeza watekelezaji nini kifanyike kwenye eneo la uongezaji viritubishi kwenye chakula. Bi. Ngegba amesema UNICEF itaendelea kutoa ushirikiano hadi kuhakikisha Mpango kazi huu umekamilika na kuendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania kutekeleza shughuli zilizoainishwa kwa Mpango Kazi huo wa Miaka 5,ili kihakikisha Watanzania wengi hususani watoto, wanawake waliopo kwenye umri wa kuzaa na vijana balehe wanapata vyakula vilivyorutubishwa ili kuwakinga na athari zitokanazo na Upungufu wa virutubishi vya vitamini na Madini. Wakizungumza wakati wa kikao kazi cha kuthibitisha mpango huo kilichofanyika Mkoani Morogoro, wadau mbalimbali walioshiriki kwenye kikao hicho wameipongeza Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Pamoja na timu iliyoshiriki katika kuandaa mpango huo hadi kufikia hatua ya mwisho kwani unaenda kusaidia kuimarisha eneo la urutubishaji nchini, na ni mpango ambao wadau wengi wa urutubishaji walikuwa wanauhitaji.