TFNC YATAMBULISHA AWAMU YA PILI YA MRADI WA KUBORESHA LISHE KWA WANAWAKE WAJAWAZITO (IMAN II)
16 Jun, 2026
TFNC YATAMBULISHA AWAMU YA PILI YA MRADI WA KUBORESHA LISHE KWA WANAWAKE WAJAWAZITO (IMAN II)
Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imetambulisha rasmi awamu ya pili ya mradi wa kuboresha lishe kwa wanawake wajawazito unaojulikana kama "Lishe Yangu" (IMAN II).   Mradi huo unalenga kupunguza changamoto za lishe na kuhakikisha wajawazito wanapata virutubishi muhimu katika kipindi chote cha ujauzito.     Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili mradi huo leo tarehe 11 Juni 2026 katika Ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, ameipongeza TFNC na wadau wote kwa hatua hiyo.   Dkt. Mfaume ameahidi kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yote yaliyokusudiwa.   Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dkt. Germana Leyna, amebainisha kuwa mradi huu awamu hii umeelekezwa zaidi katika mikoa minne ambayo ni Dodoma, Njombe, Mbeya, na Songwe.   Dkt.Germana amesema uzinduzi rasmi wa mradi wa IMAN unatarajiwa kufanyika mkoani Njombe ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Juni, 2026.   Mradi wa "Lishe Yangu" unatekelezwa chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF). Lengo kuu ni kuboresha lishe ya mama na mtoto kwa kuhamasisha utekelezaji wa kitita cha huduma muhimu za lishe.   Kupitia afua za mradi huu, wanawake wajawazito watawezeshwa kupata huduma bora za lishe ili kupunguza tatizo la upungufu wa virutubishi mwilini (micronutrient deficiency), kuboresha afya zao wakati wa ujauzito, na kuweka msingi imara wa ukuaji wa mtoto aliye tumboni.   Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali muhimu, wakiwemo Maafisa Lishe kutoka mikoa ya Dodoma, Njombe, Mbeya na Songwe, wawakilishi kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Mfamasia Mkuu, na viongozi kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu.