TFNC KWA KUSHIRIKIANA SHIRIKA LA NI YATOA MAFUNZO YA MWONGOZO WA CHAKULA NA ULAJI KWA MAAFISA LISHE WA MIKOA YA TANZANIA BARA
03 Jul, 2026
TFNC KWA KUSHIRIKIANA SHIRIKA LA NI YATOA MAFUNZO YA MWONGOZO WA CHAKULA NA ULAJI KWA MAAFISA LISHE WA MIKOA YA TANZANIA BARA
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), kwa kushirikiana na Shirika la Nutrition International (NI) pamoja na wadau wengine wa lishe, imeendesha mafunzo maalumu kwa Maafisa Lishe kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara yenye lengo la kuwajengea uwezo kuhusu Mwongozo wa Chakula na Ulaji kwa Tanzania Bara ili kuboresha utoaji wa elimu ya lishe kwa jamii. Mafunzo hayo ya siku tatu yamezinduliwa rasmi na Mkurugenzi wa Nutrition International Tanzania, Dkt. George Mwita, ambaye amewataka washiriki kuhakikisha maarifa watakayoyapata yanatumika kuleta mabadiliko chanya katika jamii, akieleza kuwa changamoto za lishe bado zinaendelea kuathiri makundi mbalimbali ya wananchi, hususan vijana rika balehe. Kwa upande wake, Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Bi. Maria Ngilisho, amesema mafunzo hayo yataendelea kwa siku tatu hadi Juni 27, 2026, yakilenga kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu mwongozo huo pamoja na namna bora ya kuutumia katika kusaidia jamii kupanga mlo kwa usahihi. Amesema matarajio ya TFNC ni kwamba baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, kila mshiriki atakuwa na uwezo wa kutafsiri na kusambaza kwa ufanisi jumbe mbalimbali zenye kuelimisha na kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia za mtinda bora wa maisha hasa ulaji. Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bw. Luitfrid Nnally  amewasisitiza maafisa lishe wanaoendelea na mafunzo kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano, ikiwemo kushirikiana na vitengo vya mawasiliano vya Serikali, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za lishe na kupunguza upotoshaji unaoendelea kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa Maafisa Lishe nchini katika kutekeleza Mwongozo wa Chakula na Ulaji, hatua itakayochangia kuhamasisha jamii kufuata kanuni za lishe bora zitakazosaidia kupunguza hatari ya kupata changamito za udumavu, upungufu wa madini na vitamini, uzito uliozidi na magonjwa sugu na hivyo kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.