Waziri Mkuu asema lishe bora ni kipaumbele cha Serikali

News Image

Imewekwa: 3rd Oct, 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa suala ya lishe ni kipaumbele muhimu kwa Serikali katika kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na shughuli za kiuchumi kwa jamii zikiwemo za kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara.

Mhe. Majaliwa amesema hayo Oktoba 03, 2024 wakati alipofunga Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika kwenye Ukumbi wa Malaika Beach Resort jijjini Mwanza

Amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe.

Hatua ambayo imemfanya awe kinara na mmoja wa viongozi wanaotambuliwa na kutolewa mfano ulimwenguni kwa hatua ambazo wameweza kupiga katika mapambano dhidi ya changamoto za utapiamlo”amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine Majaliwa ametoa wito kwa wadau wote wa lishe wahakikishe wanatumia vizuri matokea ya ripoti ya mapitio ya muda wa kati ili kujitathmini na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wa afua za lishe.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza mikoa na halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatumia mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na wahakikishe matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa yanajumuishwa na kutengewa fedha katika mipango na bajeti za kila mwaka.

“Ofisi ya Rais - TAMISEMI hakikisheni kuwa mikataba ya lishe kati ya Mheshimiwa Rais na Wakuu wa Mikoa inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija. endeleeni kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara.”amesema Majaliwa.

Kadhalika, Majaliwa amezitaka wizara, wakala, taasisi na mashirika ya umma watumie kikamilifu mwongozo wa mpango jumuishi wa Taifa wa lishe na bajeti na kuhakikisha masuala ya lishe yanajumuishwa katika mipango na kutengewa fedha ili yatekelezwe kikamilifu kila mwaka.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema wataendelea kuziratibu ipasavyo Wizara na Taasisi husika hususani zile zinazohusika na masuala ya Afya, Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda na biashara ili kuhakikisha Jamii inaelimishwa na kuhamasishwa ipasavyo juu ya lishe bora na kwamba, chakula salama chenye ubora kinapatikana kwa gharama nafuu katika Jamii yetu.

“Serikali imeendelea kuhakikisha sekta zinazohusika na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe zinaingiza masuala hayo katika Mipango na bajeti kila mwaka. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuhakikisha tunawakutanisha mara kwa mara wadau kujadili utekelezaji wa afua za lishe nchini” amesema Mhe.Lukuvi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akimkabidhi cheti cha pongezi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Bw. Anthony Mtaka, kwa kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya Utapiamlo katika mkoa wa Njombe , mara baada ya kuhitimisha Mkutano mkuu wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza kuanzia tarehe 02 hadi 03 Oktoba, 2024