Wazalishaji chumvi wadogo wasimamiwe kuzalisha chumvi iliyoongezwa madini joto

News Image

Imewekwa: 19th Jun, 2023

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe ameitaka kamati ya Taifa ya Kudhibiti Upungufu wa Madini joto nchini, kuhakikisha inasimamia na kufuatilia wazalishaji chumvi wadogo nchini kuhakikisha chumvi wanayozalisha nchini inawekewa madini joto ili kuweza kupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza kwa watumiaji wa chumvi watakaokosa madini hayo muhimu mwilini.

Dkt. Magembe amebainisha hayo wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa 55 wa Kamati ya Taifa ya Kudhibiti Upungufu wa Madini Joto nchini, ambao umefanyika tarehe 16 Juni 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania jiji Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Maghembe amesema hawana shaka na chumvi inayozalishwa na viwanda vilivyopo nchini juu ya uongezaji wa madini joto, ila kuna wazalishaji wadogo wapo ambao hawaongezi madini joto kwenye chumvi wanayozalisha, na chumvi hiyo imekuwa ikiingizwa sokoni katika maeneo yao na kutumiwa na wananchi.

“Suala la kuvuna chumvi linalofanywa na wazalishaji wadogo ni ajira na hauwezi kuwakataza wasivune chumvi ambayo inawaingizia kipato,ila ni lazima tuchakate vichwa vyetu na kuhakikisha wazalishaji wadogo hawa wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa kwa kuhakikisha chumvi wanayozalisha inawekewa madini joto.

Aidha Dkt. Magembe ameitaka kamati hiyo kuhakikisha elimu ya umuhimu wa madini joto inatolewa kwa wazalishaji chumvi wadogo, na kuwaelimisha umuhimu wa kutumia chumvi iliyoongezwa madini joto na athari za kiafya anazoweza kuzipata mtu ambaye hatotumia chumvi ambayo imeongezwa madini joto.