07 Feb, 2026
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imeingia ushirikiano wa kimkakati na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi ya matatizo ya utapiamlo nchini. Ushirikiano huo utawezesha kutumia rasilimali watu katika kufanya tafiti, kutoa mafunzo kwa pamoja, na kutengeneza bidhaa za chakula lishe.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TFNC jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka TFNC, Dkt. Esther Nkuba, amesema tafiti zitakazofanyika kutokana na ushirikiano huo zitajikita kuleta majibu ya kutatua changamoto za kilishe na hivyo kuchangia katika kuboresha hali ya lishe kwa Watanzania.
Aidha Dkt. Nkuba amesema kuwa kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) ni matokeo ya maelekezo yaliyotolewa wakati wa kikao cha COMPACT.
“Tumejipanga kuhakikisha ushirikiano huu unaleta matokeo chanya katika sekta ya lishe," alisema Dkt. Nkuba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Uuguzi na Afya ya Jamii kutoka UDOM, Dkt. Leonard Katalambula, amebainisha kuwa chuo hicho kina hazina kubwa ya wataalamu katika sekta mbalimbali ambao watakuwa chachu katika kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya pande zote mbili.
"Kupitia ushirikiano huu, TFNC ina fursa pana ya kushirikiana na wataalamu wetu katika kuboresha majukumu yake ya kila siku na kufikia lengo kuu la kutokomeza utapiamlo nchini," aliongeza Dkt. Katalambula.
Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza kasi ya tafiti za kisayansi kuhusu vyakula vya asili, uzalishaji wa vyakula dawa na vyakula vyenye virutubishi vingi kwa makundi maalumu wakiwemo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa za lishe kuanzia ngazi ya vijiji, pamoja na kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
