Watoto milioni 11 wenye umri chini ya miaka 5 nchini kupatiwa matone ya vitamini A Juni 2024
Imewekwa: 14th Mar, 2024
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikabidhi vidonge vya matone vya Vitamini A milioni 22 kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Mhe. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri ya Afya Mhe. Ummy Mwalimu.
Hafla ya makabidhiano ya vidonge vya Vitamini A kutoka Shirika la Nutrition International (NI) yamefanyika katika Ukumbi wa Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dar es Salaam ambapo Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekabidhi Vidonge hivyo kwa niaba ya Shirika la Nutrition International.
Serikali kupitia Wizara afya imepokea vidonge vya matone ya Vitamini A milioni 22 kutoka kwa Shirika la Nutritrion International kwa ajili ya kuwapatie watoto walio na umri chini ya miaka 5 wapatao milioni 11 kwa ajili ya kuongeza kinga ya mwili na kuimarisha afya ya macho kwa watoto hao
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Machi 13, 2024 Mollel wakati wa makabidhiano ya vidonge vya matone ya Vitamini A kutoka Shirika la Nutrition International (NI) jijini Dar Es Salaam.
Dkt. Mollel amesema Vidonge vya matone ya Vitamini A vitasaidia kuongeza kinga ya Mwili na kuimarisha afya ya macho kwa watoto walio na umri chini ya miaka tano.
Amesema elimu ya mtoto inaanza siku mimba inatunga na sio shuleni kwa kumpatia Mama lishe iliyo bora wakati wa ujauzito ili kusaidia kuimarisha ubongo wa Mtoto
“Wazazi zingatieni lishe bora kwa watoto tangu wa utungaji wa mimba na kuwa na desturi ya kula mlo bora kwa mama wajawazito na hii itamsaidia mtoto hata baada ya kuzaliwa na wakati yuko shule ubongo na akili yake kufanya kazi kikamilifu pia itamuepusha na magonjwa ya mara kwa mara” Dkt. Mollel amesema
Dkt. Mollel amewataka Watanzania kuzingatia milo yao ya kila siku kwa kupata chakula chenye lishe hasa vyenye vitamini ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu , magonjwa ya moyo na kisukari
Ameongeza kuwa ya Serikali ya awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha Tsh. bilioni 99 kwa ajili ya kuajiri na posho za wahudumu wa afya ngazi ya jamii pia wamekuwa msaada mkubwa wa kufikisha elimu ya lishe na afya bora kwa jamii
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya menejimenti nchini ya Shirika la Nutrition International (NI) amesema Shirika la Nutrition Internation limeipatia Serikali vidonge vya matone vya Vitamini A milioni 22 na kuongeza kuwa vitamini A umsaidia mtoto kuimarisha afya ya macho na kuongeza kinga mwilini.