Watanzania tufuate taratibu sahihi za unyonyeshaji - Waziri wa Afya

News Image

Imewekwa: 3rd Aug, 2021

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mhe. Cosmas Nshenye ameitaka jamii kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha taratibu sahihi za ulishaji wa watoto wachaga na wadogo zinafuatwa ipasavyo ili kuweza kutokomeza tatizo la udumavu nchini.

Mhe. Nshenye ametoa rai hiyo alipomuwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Mhe. Dorothy Gwajima kufungua Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani 2021 tarehe 01/08/2021 kwenye viwanja vya Vwawa CCM wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.

“Kunyonyesha maziwa ya mama kunaimarisha afya na ustawi wa wanawake na watoto na ni msingi wa maendeleo ya nchi na mustakabali wake wa baadaye pia ni njia ambayo inaleta usawa mkubwa katika kuvunja mzunguko wa umaskini nchini. Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia aina zote za utapiamlo, huhakikisha uhakika wa chakula kwa watoto wachanga na wadogo, kwa hiyo unyonyeshaji ni msingi wa maisha. Kulinda, kuendeleza na kuimalisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni jambo lenye umuhimu katika kujenga dunia na Tanzania endelevu.”

Kwenye hotuba hiyo ya Waziri wa Afya, Mhe. Dorothy Gwajima ambayo imesomwa na Mhe. Nshenye imesema kuwa licha ya Tanzania kufanya vizuri kwenye unyonyeshaji ambapo asilimia 98 ya wanawake wanachagua kuwanyanyosha watoto wao maziwa ya mama lakini bado changamoto zipo kwenye kufuata taratibu sahihi za ulishaji wa watoto wadogo na wachanga.

“Asilimia 35 tu ya watoto hupatiwa mlo kamili wenye mchanganyiko sahihi wa makundi ya vyakula, asilimia 58 ya watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanapewa idadi sahihi ya milo kwa siku kulingana na umri wao. Kwa ujumla, watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanaopewa milo yenye ubora wa kukidhi mahitaji yao kilishe ni asilimia 30 tu”

Aidha akisoma hotuba hiyo, Mhe. Nshenye amesema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani ni sehemu mojawapo muhimu inayowakutanisha wadau mbalimbali kujadili hatua stahiki za kuchukua ili kulinda na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama, hivyo tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha wiki kuanzia tarehe 01 Agosti hadi 07 Agosti kauli mbiu ya mwaka huu inasema *“Kulinda unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni jukumu letu sote”.*

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Cosmas Nshenye (wa kwanza kushoto) akisikiliza maelezo juu ya ilishaji wa watoto kutoka kwa wataalamu wa lishe wakati alipotembelea mabanda ya maonesho kwenye viwanja vya Vwawa CCM mkoani Songwe kabla ya kufungua maadhimisho hayo tarehe 01/08/2021 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima