Wananchi kijiji cha pwaga wilayani mpwampwa wapatiwa elimu ya lishe

News Image

Imewekwa: 8th Apr, 2023

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bi. Sofia Kizigo amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika ziara ya kuangalia shughuli zinazofanyika katika Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji wilayani humo, ziara ambayo imeratibiwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia ufadhili wa WFP.
Wito umetolewa kwa kina baba kuhudhuria kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) ili waweze kushiriki kupatiwa elimu ya lishe pamoja na huduma mbalimbali zinazohusiana na afya na lishe ili waweze kushiriki katika kusimamia lishe za watoto wao na kutengeneza kizazi chenye lishe bora.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bi. Sofia Kizigo wakati aliposhiriki kwenye utekelezaji wa Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI), akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu, na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika katika siku hiyo ambayo utekelezwa kila baada ya miezi mitatu.

Kizigo amesema katika Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) kumekuwa kunatolewa huduma mbalimbali zinazohusu masuala ya afya na lishe na kina mama wengi wamekuwa wakiudhuria kupata huduma hizo huku kina baba wakiwa nyuma, hivyo ni jukumu lao kushirikiana na akina mama na kuhakikisha watoto wao wanapatiwa huduma hizo. “ili kutengeneza kizazi chenye lishe bora tunachokitaka ni lazima tuwekeze kwenye lishe na kuhakikisha tunapata elimu sahihi ya lishe ambayo itatusaidia katika kutengeneza kizazi chenye lishe bora.”amesema Kigozi.
Aidha katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wanawake wanapohisi wajawazito kuanza kuhudhuria kliniki mara moja, ili kuhakikisha siku 1000 za makuzi ya mtoto zinazingatiwa na kuwezesha kuwa na taifa lenye watu wenye afya na lishe bora na kuweza kufikia malengo endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema Taasisi hiyo iliandaa ziara ya Mhe.Waziri kushiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI) ili kuweza kujionea shughuli zinazofanyika katika siku hiyo, na namna gani zimekuwa zikisaidia katika utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe. Dkt. Germana amemuomba pia Bi. Kizigo ambaye amemwakilisha Waziri wa Afya kuhamasisha jamii ya watanzania juu ya umuhimu wa lishe bora kwani lishe ndiyo msingi wa kila kitu, na hatuwezi kuwa na maendeleo kama wananchi wake hawana lishe bora.