Wanafunzi wasioona shule ya msingi mgeza mseto bukoba wapatiwa vitabu vya braille na radio zenye ujumbe muhimu wa lishe

News Image

Imewekwa: 8th Apr, 2024

Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imekabidhi vitabu 30 na radio 50 zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona vilivyoandaliwa kwa maandishi ya nukta nundu (Braille) kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wasioona shuleni hapo.

Nyenzo hizo muhimu kwa watu wasioona zimekabidhiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) Bw. Omary Itambu kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mseto na vitatumiwa na wanafunzi wasiona kujifunza na kupata elimu sahihi ya masuala mbalimbali ya lishe kwa kusoma kupitia maandishi ya nukta nundu na kusikiliza kupitia ujumbe wa sauti uliorekodiwa katika redio.

Bw. Itambu amesema awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa na elimu sahihi ya masuala ya afya na lishe kutokana na aina ya ulemavu walionao hivyo kujiona kama kundi ambalo limetengwa katika kupata taarifa hizo muhimu.

“hizi ni nyenzo muhimu ambazo tunazikabidhi shuleni kwa ajili ya vijana wetu wasioona kupata elimu ya lishe, ambayo awali walikuwa wanaikosa. Kujifunza kwao kwa sasa kutasaidia kuwafanya kuwa na elimu pana kuhusu masuala ya Chakula na Lishe.” Alisema Itambu

Akipokea vitabu hivyo vyenye maandishi ya nukta nundu na radio zenye ujumbe muhimu wa lishe, kwa niaba ya Afisa Elimu Maalumu Manispaa ya Bukoba, Afisa elimu Taaluma wa Manispaa hiyo Bi Upendo Nanyaro amesema nyezo hizo ni muhimu sana kwa wanafunzi wasioona kwani ndiyo mwanzo wa kuweza kuwasaidia kujua na kutambua masuala muhimu yanayohusiana na Chakula na Lishe.

Kwa Upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto Bi. Augustina Daniel ameishukuru Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kuwasaidia nyezo hizo muhimu, hivyo kuanzia sasa wanafunzi wake wataweza kupata elimu sahihi ya masuala ya afya na lishe kama ilivyo kwa makundi mengine.