Waandishi wa habari toeni elimu sahihi zinazohusiana na masuala ya chakula na lishe
Imewekwa: 27th Sep, 2024
Waandishi wa habari mbalimbali nchini Tanzania wametakiwa kuandika na kuziwasilisha kwa weledi habari zinazohusu masuala ya chakula na lishe kwa jamii ya Watanzania, na kuachana na zile zisizo sahihi ambazo zimekuwa zikizua taharuki kwenye jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Esther Nkuba, Septemba 26, 2024 wakati akifungua semina kwa waandaji wa vipindi, watangazaji na waandishi wa habari, ambayo ililenga kuwajengea uwezo katika kuripoti kwa ufasaha taarifa kuhusu masuala ya chakula na lishe.
Dkt. Nkuba amesema waandishi wa habari wana mchango mkubwa katika kuelimisha masuala mbalimbali yanayohusiana na lishe na kuchochea mabadiliko ya tabia za ulaji kwa jamii ya watanzania.
“Waandishi wa Habari kama nyie mna mchango mkubwa sana katika kuelimisha Taifa na hata kusaidia kufikia hatma ya uchumi endelevu, kwa sababu mtu akiwa na afya na lishe bora, ataweza kufanya vizuri katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na ujenzi wa taifa.
Aidha Dkt. Nkuba amesema wapo baadhi ya waandishi wanaotoa taarifa zisizo sahihi zinazohusiana na masuala ya chakula na lishe na kuleta taharuki kwenye jamii, na hiyo inasababishwa kwa wao kutozingatia chanzo sahihi cha habari ilhali kuna Taasisi rasmi yenye jukumu la kutoa taarifa sahihi.
Kwa upande wake Afisa Lishe Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Bi. Maria Ngilisho, amewataka wanahabari hao kuzingatia utoaji wa taarifa sahihi zinazohusiana na masuala ya lishe, kwani kufanya hivyo kutasaidia jamii kufuata njia za sahihi zinazohusiana na masuala ya ulaji.