Virutubishi vinavyoongezwa kwenye chakula sasa kuanza kuzalishwa nchini

News Image

Imewekwa: 3rd Jun, 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, amesema Tanzania inatarajia kuachana na kuagiza Virutubishi vinavyoongezwa kwenye vyakula nje ya nchi na badala vitapatikana hapa hapa nchini baada ya Shirika la SANKU kujenga kiwanda cha kutengeneza virutubishi hivyo kilichopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mhagama amebainisha hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea namna kitavyoweza kuendesha shughuli zake,ambapo amesema kitakuwa ni kiwanda pekee kwenye ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kati kitakachokuwa kinazalisha virutubishi vinavyoongezwa kwenye chakula.

“Muda mrefu ilikuwa ni ndoto ya Serikali kuwa na kiwanda kinachozalisha viritubishi kitakachopatikana ndani ya nchini, na suala hili tuliweza kuiachia sekta binafsi na leo hii tunaenda kuwa na kiwanda chetu wenyewe kinachoenda kuzalisha virutubishi ndani ya nchi na vinaenda kusaidia suala la urutubishaji wa vyakula nchini.Amesema Mhe. Mhagama

Waziri Mhagama ameongeza kuwa uanzishwaji wa kiwanda hicho utasaidia uongezaji wa ajira kwa Watanzania ambao bado wapo kwenye soko la ajira, huku akiwapongeza SANKU kwa maamuzi yao ya kuhakikisha asilimia 80% ya Malighafi zitakazotumika kutengeneza virutubishi hivyo zitatoka hapa hapa nchini.

Shirika la SANKU kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wamekuwa wakiendelea kuwasaidia wasindikikaji wadogo wa unga kupata virutubishi na vifaa vya kufanyia urutubishaji pamoja na kuhamasisha wasindikizaji hao kuzalisha unga uliongezwa virutubishi vya madini na vitamini ili kuweza kukabiliana na matatizo ya upungufu wa viritibishi hivyo muhimu mwilini.