Utafiti wa FORTIMAS awamu ya pili kuendelea katika mikoa ya Dar es salaam, Mtwara na Singida

Imewekwa: 15th Mar, 2025
Watafiti kutokaTaasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) pamoja na Wataalamu wa Masuala ya athari za kiafya za upungufu wa madini joto mwilini kutoka Shirika la Iodine Global Network (IGN) Tanzania, wamefanya ziara katika Mkoa wa Dar Es Salaam, Mtwara na Singida na kufanya majadiliano na kupeana maelekezo na watendaji wa ngazi za Mkoa na Halmashauri kuhusu namna ya kuendeleza utekelezaji wa utafiti wa programu ya chumvi (FORTIMAS) awamu ya pili unaolenga kuangalia uwezekano wa kutumia mfumo wa ufuatiliaji viwango vya madini joto mwilini na katika chumvi (USI surveillance System).
Kukamilika kwa utafiti huu kutaiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza Afrika kupima hali ya viwango vya madini joto katika jamii kwa wakati kwa kutumia mifumo endelevu badala ya kusubiri tafiti za kitaifa zinazofanyika kila baada ya miaka mitano.
Pamoja na mambo mengine watafiti hawa wameweza kuwapatia matokeo ya awali ya taarifa zalizokusanywa katika awamu ya kwanza kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2024. Vile vile, ugawaji wa vifaa maalumu kwa ajili ya kukusanya sampuli za utafiti huu vimetolewa katika vituo vya afya 12 pamoja na shule za msingi 12 zilizochaguliwa kushiriki katika utafiti huu ambazo zipo katika Halmashauri za Manispaa ya Ilala na Temeke Mkoa wa DSM; Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na Nanyumbu DC Mkoa wa Mtwara, na Halmashauri ya Manispaa ya Singida na Ikungi DC Mkoa wa Singida.
Uchambuzi wa kimaabara wa viwango vya madini joto mwilini na katika sampuli za chumvi utafanyika katika maabara za Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania.