Umakini uzingatiwe katika utoaji wa taarifa za masuala ya lishe

News Image

Imewekwa: 4th Jun, 2025

Vyombo vya habari vimetakiwa kuwa makini katika kuandika au kurusha maudhui yanayopotosha jamii kuhusu lishe sahihi “kwani lishe bora si suala la afya pekee, bali ni msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.”

Hayo yamesemwa na Geoffrey Chiduo, Afisa Utafiti Mchumi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TNFC), wakati akiwasilisha mada kuhusu Juhudi za Serikali katika Kuboresha Hali ya Lishe Tanzania kwa waandishi wa habari na wahariri katika semina iliyoandaliwa na Jukwaa la Lishe Tanzania (PANITA).

Semina hiyo iliangalia hali ya lishe nchini, juhudi za serikali katika kuimarisha lishe bora (Nutrition for Growth) na nafasi ya vyombo vya habari katika kuboresha hali ya lishe kwa jamii.

Chiduo ametoa mfano wa kituo kimoja cha televisheni ambacho hakukitaja, kilichomhoji msanii mmoja akijitapa kwa kunyonyesha mtoto kwa wiki mbili! Hii amesema ni hatari kwa afya ya mtoto kwani hali ya lishe duni, ikiwemo watoto kutonyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na kuendelea hadi miaka miwili huku wakichanganyiwa na vyakula vingine, huchangia udumavu. Ametoa mfano mwingine wa chombo cha habari kilichorusha habari ya mtu aliyedai masuala ya kuzingatia lishe kiafya ni masuala ya Wazungu!

Wanahabari katika semina hiyo wamejifunza kwamba katika siku 1,000 za mwanzo za maisha ya mtoto, kutoka mimba hadi miaka miwili, lishe duni husababisha udumavu usioweza kurekebishwa baadaye. Kwamba udumavu huleta madhara makubwa kiafya, kielimu, na kiuchumi hata mtoto anapofikia utu uzima bado huwa na athari nyingi katika utendaji kazi wake. Hali hii inadhihirisha kuwa, bila lishe bora, hakuna afya bora, na bila afya bora, hakuna Taifa lenye tija.