08 Oct, 2025
Ujumbe wa wataalamu wa kutoka Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane, Wizara ya Uchumi na Wizara ya Afya kutoka nchini Msumbiji, umeendelea na ziara yake nchini ambapo jana Oktoba 7,2025 wajumbe hao walitembelea mashamba ya walizalishaji chumvi yaliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yao ya kujifunza na kupata maarifa juu ya utekelezaji wa mpango wa kuzuia upungufu wa madini joto (USI) kama mkakati wa muda mrefu wa kuzuia na kudhibiti upungufu wa madini joto mwilini.
Wataalamu hao wameweza kujionea na kujifunza namna wazalishaji chumvi hao wadogo na wale wa kati namna wanavyoshirikiana na serikali katika utekelezaji wa mpango wa kuzuia upungufu wa madini joto ( USI) kwa kuhakikisha chumvi wanayozalisha inawekewa madini joto ya kutosha kabla ya kuingia sokoni kwa ajili ya watumiaji.
Wataalamu hao watakuwa nchini Tanzania kwa muda wa siku tano ambapo mbali na kutembelea wazalishaji wa chumvi katika mashamba ya chumvi pia wanatarajia kutembelea maabara ya Chakula na Lishe ya TFNC kujifunza namna inavyofanya kazi zake katika uchambuzi wa sampuli mbalimbali za vyakula na zile za kibaolojia pamoja na kutembelea baadhi ya vituo vilivyohusika kwenye utafiti wa majaribio ya Mfumo wa Utuatiliaji wa Takwimu za Chumvi (FORTIMAS) jijini Dar es Salaam.
