07 Oct, 2025
Tarehe 6 Octoba, 2025 Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imepokea wageni kutoka Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane, Wizara ya Uchumi na Wizara ya Afya kutoka nchini Msumbiji, kwa lengo la kujifunza na kupata maarifa juu ya utekelezaji wa mpango wa kuzuia upungufu wa madini joto ( USI) kama mkakati wa muda mrefu wa kuzuia na kudhibiti upungufu wa madini joto mwilini.
Ziara hii itatoa fursa nzuri kwa wataalam hao kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushirikiana moja kwa moja na wadau wa lishe wa Tanzania na wale wa kimataifa wanaohusika na mpango wa USI.
Katika ziara hiyo ya kujifunza, Wataalamu hao watakuwa nchini Tanzania kwa muda wa siku tano ambapo watapata fursa ya kutembelea maabara ya Chakula na Lishe ya TFNC kujifunza namna inavyofanya kazi zake katika uchambuzi wa sampuli mbalimbali za vyakula na zile za kibaolojia. Pia watapata fursa ya kutembelea wazalishaji wa chumvi katika mashamba ya chumvi na viwanda vya kuchakata chumvi, ili kupata uzoefu wa uzalishaji na usindikaji chumvi katika mnyororo wa thamani.
Vilevile, Wataalamu hao watatembelea baadhi ya vituo vilivyohusika kwenye utafiti wa majaribio ya Mfumo wa Utuatiliaji wa Takwimu za Chumvi (FORTIMAS) jijini Dar es Salaam.
