Ufunguzi wa mafunzo kwa wadau na wataalamu wa Urutubishaji vyakula nchini

News Image

Imewekwa: 14th Apr, 2025

Wizara ya Viwanda na Biashara, imesema dhamira ya serikali ni kuona Watanzania wanapata vyakula ambavyo vina ubora kilishe lakini vyenye virutubishi muhimu kwa ustawi wa afya zao.

Hayo yamebainishwa na Afisa Biashara Mwandamizi Kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Festo Kapela kwa niaba ya Katibu Mkuu, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wadau na wataalamu wa Urutubishaji vyakula kutoka maeneo mbalimbali nchini yanayofanyika Mkoani Morogoro

Mafunzo hayo ya siku nne yameandaliwa na Jukwaa la Wadau wa Uongezaji Virutubishi kwenye vyakula nchini (The Tanzania Food Fortification Alliance) (TFFA), Wizara ya Viwanda na Biashara , Wizara ya Afya ,Taasisi ya Food Fortification Initiative (FFI) , Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania chini ya uwezeshaji kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF).

Kapela amesema mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha afua ya uongezaji virutubishi kwenye vyakula na tayari kama nchi tayari,Aprili 3, mwaka huu zimezunduliwa kanuni ambazo zinaenda kutumika na lengo kubwa ni kuhakikisha unawekwa ulazima katika suala la uongezaji virutubishi kwenye chakula .

“ kabla sheria na kanuni hizi wazalishaji wa vyakula kulikuwa na kulaumiana ya kwamba baadhi walikuwa wakiwema virutubishi lakini wengine hawaweki na kulifanya jambo kuwa ngumu katika utekelezaji wake “amesema Kapela

Mbali na hayo alisema suala la lishe na chakula linaenda katika nyanja kadhaa kwani ni afya , maisha lakini pia ni uchumi na hivyo kuziomba sekta binafsi zinazojihusisha na uzalishaji wa vyakula kutekeleza suala hilo.

Akiwasilisha salama kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Luitfrid Nnally , ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kutunga sheria na kupitisha kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula ili viwe na ubora katika kusaidia kupambana na matatizo ya lishe kwa watoto na jamii ya watanzania .

“ Tumekutana hapa katika mafunzo haya kwa ajili ya kujadili mikakati hii , na sina budi kwanza kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye suala la lishe amelipa kipaumbele kikubwa na kauli mbiu yake “ Tanzania bila utapiamlo inawezekana “ alisema.

Nnally alisema kuwa kipaumbele hicho ni tangu alipokuwa Makamu wa Rais ambapo aliweza kusainisha mikataba na wakuu wa mikoa waweze kuhakikisha ya jamii inakuwa na lishe bora.

Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema baada ya mafunzo hayo ,jukumu kubwa kwa watendaji na wadau mbalimbali wenye mamlaka ni ufuatiliaji kwa wataalamu waongezaji virutubishi kwenye vyakula ili kuona ubora wa vyakula unakuwa wa viwango vya juu .

Alitaja eneo lingine ni kuangalia wasindikaji wa vyakula endapo wanazingatia viwango vilivyowekwa kitaifa kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa na matokeo mazuri ya kiafya yanayotokana na ulaji wa vyakula hivyo .

“ Ufuatiliaji itafanyika kwenye meneo ya ndani ya viwanda au ndani mzalishaji wa hicho chakula kwa kuangaliwa ubora wa malighafi zinazotumika kuongezea virutubishi , mchakato wa usindikaji uzingatie viwango, eneo la uonjaji na kupima ubora wa kile kinachozalishwa ” alisema Nnally.