Tumieni taaluma zenu kutatua changamoto za masuala ya chakula na lishe kwenye jamii

News Image

Imewekwa: 26th Sep, 2023

Na Mwandishi wetu-TFNC Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna, amefungua mafunzo elekezi kwa Waajiriwa wapya wa Taasisi, ambapo amewataka kutumia taaluma zao katika kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za masuala ya chakula na lishe zinazoikabili jamii.
Dkt. Germana amesema mafunzo hayo ya siku tano yamelenga kuwawezesha waajiriwa hao kujua mifumo mbalimbali ya kiutumishi, itakayowasaidia katika kutatua changamoto hizo, na kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo Taasisi imekabidhiwa na Serikali kuyatekeleza. “Mimi matarajio yangu kwenu ni makubwa sana, mnisaidie kutatua changamoto za chakula na lishe kwa jamii na ndiyo changamoto ambazo sisi kama Taasisi ni jukumu ambalo tumekabidhiwa na Serikali ili kuweza kulitekeleza.” amesema Dkt. Germana
Aidha Dkt. Germana amewataka waajiriwa hao kutokuwa sehemu ya walalamikaji kwa changamoto zilizopo ndani ya Taasisi bali wawe sehemu ya suluhisho ya changamoto hizo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Fedha,Utumishi na Utawala Bw. Ally Said, amewataka watumishi hao kuzingatia mafunzo wanayopatiwa kwani yatakuja kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Taasisi. Kwa mujibu wa waraka namba 5 wa mwaka 2011 wa Utumishi, unaelekeza kila waajiriwa wapya ni lazima wapatiwe mafunzo elekezi ili kuwawezesha kufahamu uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi husika, pamoja na kufahamu sheria mbalimbali za utumishi na utawala bora.