Timu ya Watafiti bobezi kutoka TFNC pamoja na IGN watoa mafunzo mkoa wa Singida
Imewekwa: 30th Sep, 2024
Timu ya Watafiti bobezi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) pamoja na Iodine Global Network (IGN) wametembelea mkoa wa Singida na kutoa mafunzo elekezi ya namna ya kufanya utafiti wa majaribio ya mfumo wa ufuatiliaji taarifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto (FORTIMAS) katika ngazi ya Jamii.
Watafiti hao wamewajengea uwezo wataalamu mbalimbali kutoka ngazi ya Mkoa na halmashauri za Singida mjini na Ikungi wakiwemo Waganga wakuu, Maafisa Lishe, Waratibu wa Mama na Mtoto, Wauguzi, Wataalamu wa Maabara na Wataalamu wa taarifa za afya na lishe.
Pamoja na mafunzo hayo, wataalamu hawa waliwezeshwa/ walipatiwa vifaa mbalimbali vya kukusanya na kuhifadhi sampuli za chumvi na mkojo kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kimaabara kutambua viwango vya madini joto katika sampuli hizo.
Matokeo ya utekelezaji ya utafiti huu yatasaidia kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa taarifa za matumizi ya chumvi yenye madini joto ngazi ya Kaya kwa wakati na urahisi zaidi.